Home Habari za michezo STAA HUYU WA SIMBA ANAJUTA KUONDOKA YANGA, STORI KAMILI IKO HIVI

STAA HUYU WA SIMBA ANAJUTA KUONDOKA YANGA, STORI KAMILI IKO HIVI

Kuna msemo wa kukosea ni wakati wa kwenda sio kurudi. Hii ni kauli inayomlenga Gadiel Michael ambaye amezitumikia timu tatu kubwa za Ligi Kuu Bara.

Gadiel alianzia Azam FC iliyomlea na kumpa mwanga kuonekana zaidi kwa timu za Kariakoo akianza kukipiga Yanga misimu miwili na baadaye Simba.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na staa huyo ambaye ana uhakika wa namba Singida Big Stars (SBS)na kafunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujutia uamuzi wa kutoka Jangwani na kutua Simba.

ANAVYOJUTA

Gadiel alitua Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Azam FC na kuingia kikosi cha kwanza moja kwa moja akimuweka benchi Juma Abdul aliyedumu hapo kwa muda mrefu.

“Katika maisha yangu ya soka kitu ambacho sitakaa nikakisahau ni kuondoka Yanga baada ya kuitumikia kwa miaka miwili na kutua Simba nikiamini nitatimiza malengo yangu,” anasema.

“Kuondoka Yanga halafu nilipokwenda sikufikia malengo niliyotarajia ni moja ya tukio ambao sitakaa nikalisahau kwani lilinipotezea mwelekeo. Nashukuru nimerudi kwenye mstari na naanza kujitafuta upya.”

BOCCO KAMA KAKA

Nahodha wa Simba, John Bocco mbali na kujiwekea rekodi nzuri uwanjani, pia ni miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwapa moyo wachezaji wengi ambao wanakosa nafasi ya kucheza na hata wanaopitia wakati mgumu kiuchumi wamekuwa wakimuona, na hilo limethibitishwa na Gadiel.

“Bocco alikuwa mtu wa karibu yangu sana mara nyingi ndio alikuwa ananipa moyo wa kuvumilia kwasababu aliamini siku zote nina kitu licha ya kukosa nafasi ya kucheza ndani ya kikosi cha Simba,” anasema.

“Aliamini katika uwezo wangu ndani ya kikosi cha Simba, lakini muda ulipofika hakuwa na budi kukubali uamuzi wangu wa kuondoka Simba. “Alikuwa ananiambia kucheza kwangu ni suala la muda. Kauli yake ilikuwa inanipa matumaini na moyo nikiamini ipo siku nitapewa nafasi na kucheza. Sijawahi kukata tamaa kwenye maisha yangu ya soka kwa sababu ndio kazi Mungu amenipa na familia yangu inapata kula kupitia mpira. Hata wao walikuwa sehemu ya kunipa imani.”

ILIKUWA SUALA LA MUDA

Wakati wadau wengi wakihoji ilikuwaje beki huyo alijiunga na Singida Big Stars licha ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara ndani ya Simba, mwenyewe anafunguka kuwa lilikuwa ni suala la muda tu kwani walikuwa wanamhitaji muda mrefu.

“Mchezaji anatakiwa kupata nafasi ya kucheza ili aimarike zaidi. Nilichukua uamuzi wa kutua SBS iliponihitaji toka nina mkataba na Simba, lakini viongozi waligoma kunitoa. Mkataba ulivyoisha nikaongea nao na kuwaambia kijana wenu naombeni nisogee (mbele) nikapate changamoto mpya ndio nikaondoka sikutaka kuongeza tena mkataba.

“Licha ya kukosa nafasi, lakini naomba kukiri kwamba nilifanya mazungumzo mapya na viongozi wakitaka kuniongeza mkataba, lakini kwa kuwa nilikuwa nahitaji kupata nafasi ya kucheza niliomba kuondoka. Nashukuru Mungu nilikubaliwa, sasa najivunia maendeleo yangu ndani ya timu hii kwani nacheza,” anasema Gadiel.

SIRI YA UBORA

Wakati kuna watu ukiwa nao wanaona huna maana, kuna wengine walio mbali na wewe wanatamani kukupata na hiki ndicho kilichomtokea Gadiel ambaye anakiri kuwa nafasi yake ya kucheza ilikuwa ni suala la muda kwani anamini ana uwezo mkubwa. “Kitu cha ziada zaidi kujitunza, kufanya mazoezi kwa bidii, nidhamu, na kujua nini nimekifuata ndani ya timu, kwa sababu nimetoka kuaminiwa nikaingia timu ambayo sikupata nafasi sasa najitafuta baada ya kupata nafasi,” anasema Gadiel.

“Nafasi niliyoipata SBS siwezi kuichezea nitapambana hadi tone la mwisho kuhakikisha nafikia malengo baada ya kushindwa nilikotoka.”

KUCHEZA KIUNGO

Baadhi ya wadau wa soka wamemfahamu Gadiel kutokana na nafasi yake ya beki anavyoitendea haki akizitumikia timu tatu kwenye nafasi hiyo, lakini akiwa SBS ameshangaza wengi baada ya kucheza kiungo mkabaji kwa ubora akifunguka kuwa haikuwa rahisi.

“Kucheza kiungo mkabaji (namba 6)ilikuwa mara ya kwanza katika mechi za ushindani mkubwa, lakini sikucheza tu bali mwalimu aliniandaa vyema kuitumikia namba hiyo siku ya mchezo,” anasema.

“Haikuwa rahisi nilipewa taarifa kabla na kuandaliwa kuwa kwenye mchezo ule nitacheza nafasi tofauti na niliyozoea. Namshukuru Mungu nilicheza vyema na kuisaidia timu ushindi nyumbani.”

KINACHOIKWAMISHA SBS

Singida Big Stars ina wachezaji wengi wazuri na wenye majina makubwa, lakini wameshindwa kuendana na kasi ya ushindani kwenye ligi na mashindano ya kimataifa, lakini nahodha wa timu hiyo anafunguka.

“Nadhani kilichotuondoa kwenye mashindano ya kimataifa ukiwa ni msimu wetu wa kwanza kushiriki ni kukosa uzoefu. Ukiachilia mbali kushiriki kwa mara ya kwanza pia timu ina mchanganyiko wa wachezaji. Kuna ambao wana uzoefu na wengine hawana hiyo inaweza kuwa sababu kubwa ya kushindwa kufikia malengo lakini tunaamini tuna nafasi ya kuendelea kujifunza,” anasema Gadiel ambaye ni nahodha.

SINGIDA NI SHANGWE

Wakati baadhi ya mastaa waliotoka Simba na Yanga wanaendelea kusugua benchi SBS, unaambiwa Gadiel kwake ni raha tu. “Ndani ya SBS kila kitu kipo sawa na ninayafurahikia maisha yangu ya soka. Furaha ya maisha ya soka inakuja pale unapopata nafasi ya kucheza kwa sababu soka ndio maisha yako.

“Amani na furaha ndani ya timu haijalishi utakuwa wapi kikubwa uwe na furaha na unafanya kazi yako kama inavyotakiwa hiki ndicho nachokifanya ndani ya timu.”

SOMA NA HII  MANJI NDANI YA MKUTANO WA YANGA LEO JUNI 27

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here