Home Habari za michezo WAKATI DR CONGO WAKIFURAHI….LIGI YA BONGO IKO AFCON NA INONGA….ISHU NZIMA IKO...

WAKATI DR CONGO WAKIFURAHI….LIGI YA BONGO IKO AFCON NA INONGA….ISHU NZIMA IKO HIVI…

Habari za Michezo

MICHUANO ya Mataifa ya Afrika (AFCON) inaendelea kushika kasi nchini Ivory Coast ambapo kwa sasa imefikia hatua nzuri zaidi na ya kuvutia baada ya kushuhudia timu nne zikitinga nusu fainali zitakazoanza kuchezwa Jumatano ya Februari 7.

Michuano hii iliyoanza rasmi Januari 13, mwaka huu inatarajiwa kufikia tamati Februari 11 huku timu nne tayari zimetinga hatua ya nusu fainali ambazo ni wenyeji, Ivory Coast, DR Congo, Afrika Kusini na Nigeria.

Wakati michuano hii inaanza, huko Ivory Coast walikuwapo wachezaji 18 wanaocheza Ligi Kuu Bara ambao walikuwa wakiwakilisha timu zao za taifa katika Afcon hii ya 34. Ila hadi kufikia hatua hii ya nusu fainali, wachezaji 17 tayari wameshafungasha virago vyao na hivyo kumwacha mwamba mmoja tu akiendelea kutamba huko mitaa ya Abidjan ambaye ni beki wa kati wa Simba, Henock Inonga anayechezea kikosi cha DRC Congo.

Congo iliyokuwa kundi moja la ‘F’ na timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Zambia na Morocco, imefika nusu fainali baada ya kuitoa Guinea kwa mabao 3-1.

Kipa wa Yanga na timu ya taifa ya Mali, Djigui Diarra naye alijikuta akitolewa na wenyeji Ivory Coast katika hatua ya robo fainali baada ya kuchapwa mabao 2-1, kwenye dakika 120 kufuatia miamba hiyo kufungana bao 1-1, ndani ya dakika 90.

Kwa mantiki hiyo Ivory Coast itacheza na DR Congo Jumatano hii huku Inonga pekee akiendelea kupeperusha bendera ya Ligi Kuu Bara.

Nyota 17 wa Ligi Kuu Bara waliotolewa ni Aishi Manula, Beno Kakolanya, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Dickson Job, Kibu Denis, Lusajo Mwaikenda, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Abdulmalick Zakaria, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mzamiru Yassin, Sospeter Bajana na Mudathir Yahya waliokuwa wanapeperusha bendera ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’ iliyotolewa hatua ya makundi tu.

Wengine ni Clatous Chama, Kennedy Musonda waliokuwa na Zambia, Djigui Diarra (Mali) na Stephane Aziz KI wa Burkina Faso.

SOMA NA HII  SKUDU,KONKON NA YANGA KUNA KITU HAKIPO SAWA HAPA

1 COMMENT