Home Habari za michezo CHAMA:- HAWA AL AHLY WAKIWA KWAO SIO POA …ILA KITAELEWEKA TU…

CHAMA:- HAWA AL AHLY WAKIWA KWAO SIO POA …ILA KITAELEWEKA TU…

Habari za Simba leo

Kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama amesema wanakwenda kushambulia ili kupata matokeo dakika za mapema licha ya mlima mrefu walionao katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji Al Ahly utakaopigwa keshokutwa, Ijumaa huko Cairo, Misri.

Simba itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa kwanza kwenye uwanja wake wa nyumbani baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0.

Chama amesema hawatarajii mteremko, bali wanategemea ugumu dakika zote 90 na wanajiandaa kwenda kushindana bila kujali matokeo yaliyopita, huku akiweka wazi kuwa hawaendi kujilinda, bali watafunguka ili wapate matokeo dakika za mapema.

“Kupoteza kwenye uwanja wetu wa nyumbani ni sehemu ya matokeo na haitufanyi tukubali kushindwa. Bado tuna dakika 90 ngumu ugenini kama wenzetu waliweza kutufunga nyumbani na sisi tuna nafasi ya kuwafunga kwao,” amesema.

“Tulicheza vizuri uwanja wa nyumbani hatukuwa na bahati tunakwenda Misri kushambulia na kuhakikisha tunapata matokeo dakika za mapema za mchezo ili kuturudisha kwenye ushindani.”

Chama amesema wanawaheshimu wapinzani wao huku wakiwa na mbinu za kuhakikisha wanakuwa imara dakika za mapema ili kujitengenezea mazingira ya kufanya kitu kitakachowapa nafasi ya kusonga hatua inayofuata.

“Benchi la ufundi limeona upungufu tuliofanya na tayari limeanza kufanyia kazi kabla ya mchezo huo muhimu kwetu ambao utatupa nafasi ya kusonga hatua inayofuata endapo tutafanyia kazi yale ambayo tayari tumeanza kuelekezwa,” amesema.

“Tuna kocha mwenye uzoefu ambaye ametoka kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika ukichanganya na wachezaji ambao tumepata nafasi ya kucheza hatua ya robo fainali zaidi ya misimu miwili kuna kitu kimeongezeka.”

Simba ilianza mazoezi juzi na kesho inaanza safari kwenda Misri tayari kwa ajili ya kusaka kutinga hatua inayofuata.

SOMA NA HII  HIVI NDIVYO KLABU MATAJIRI WA MOROCCO, WALIVYOAMUA KUISAIDIA SIMBA ILI WAIMALIZE BERKANE KESHO...