Home Habari za michezo ROBERTINHO:- SIMBA WAKIFUNGWA NA YANGA TENA WASIMFUKUZE BENCHIKHA…

ROBERTINHO:- SIMBA WAKIFUNGWA NA YANGA TENA WASIMFUKUZE BENCHIKHA…

Habari za Simba leo

Simba inatarajiwa kushuka uwanjani kesho mjini Singida kukabiliana na Ihefu (Singida Black Stars) katika mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini wikiendi ijayo itakuwa na kibarua cha Kariakoo Derby kukabiliana na Yanga, likiwa ni pambano la kwanza kwa kocha Abdelhak Benchikha dhidi ya Miguel Gamondi.

Hata hivyo, kabla ya pambano hilo la Derby, huku Simba ikiwa na kumbukumbu ya kupigwa 5-1 na Yanga katika Derby iliyopita iliyopigwa Novemba 5 mwaka jana, kocha Benchikha amepata mtu wa kumkingia kifua kutokana na matokeo iliyopata timu hiyo katika mechi tatu zilizopita za mashindano.

Kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyekuwepo wakati Yanga ikishinda 5-1 na kutemeshwa kibarua amemkingia kifua Benchikha akisema matokeo mabaya iliyopata timu hiyo kwa sasa imetokana na usajili mbovu uliofanyika mapema, lakini ana nafasi ya kusahihisha makosa Aprili 20.

Simba na Yanga zitavaana katika pambano hilo la marudiano la Ligi Kuu litakalopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku timu hizo zikiwa zimeachana kwa tofauti ya pointi saba, Vijana wa Jangwani wakiwa nafasi ya kwanza na pointi 52 kupitia michezo 20, huku Wekundu wakiwa wa tatu na pointi 45 katika mechi 19 walizocheza, wakati Azam ikiwa ya pili na alama 47 katika mechi 21 ilizocheza.

Wekendu hao wamekuwa na matokeo yasiyoridhisha kwa kipindi cha siku za hivi karibuni kwani wametolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kupokea kipigo cha jumla cha mabao 3-0 mbele ya Al Ahly ya Misri ikilala nyumbani 1-0 na kupasuka 2-0 ugenini na kung’oka kwenye robo fainali ya michuano hiyo.

Baada ya kipigo hicho Simba ilirejea nyumbani na kutolewa tena katika hatua ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa penalti 6-5 na Mashujaa, ikiwa ni mara ya pili kwani mwaka 2018 timu hiyo ya jeshi pia iliwatoa Wekundu wa Msimbazi katika 64 Bora kwa mabao 3-2 na kuibua kelele kwa mashabiki wa klabu hiyo.

Hata hivyo, akizungumza kocha Robertinho amesema, Simba kwa sasa inalaumiwa sana lakini ukweli ni kwamba moja ya shida kubwa iliyonayo timu hiyo ni kutokaa muda mrefu na makocha jambo ambalo lina madhara makubwa kwa timu na wachezaji kwa ujumla.

Robertinho alisema hata kwa sasa akilaumiwa Benchikha kwa matokeo iliyonayo Simba ni kumuonea kwani ana muda mchache tangu ajiunge na timu na kukuta timu imeshasajili wachezaji ambao analazimikia kuwatumia hivyo hivyo kwa mifumo aliyonayo.

Amesema ukiachana na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja bado walishindwa kuziba pengo la wachezaji hasa wale waliopita kama mshambuliaji Jean Baleke na kuzidi kuifanya timu kuwa na wakati mgumu inapokuwa uwanjani.

“Sio sahihi kwa kocha kufukuzwa akiwa amepoteza mechi moja, hiyo inaonyesha kuwa hakuna idara inayomwajibisha na kusimamia malengo yaliyowekwa hapo wakati kocha huyo alipokuwa anaanza kazi bila kusahau kufanya tathimini ya kile kilichofanywa kwenye msimu na sio mechi,” amesema Mbrazili huyo ambaye alipoteza mchezo huo wa kwanza dhidi ya Yanga baada ya kuiongoza katika mechi 17 kabla ya kutimuliwa na kuletwa Benchikha.

“Kama Simba itapoteza mechi dhidi ya Yanga basi wasifanye haraka ya uamuzi na wakiruhusu hivyo basi itakuwa wamejiweka kwenye wakati mgumu wa kuchukua ubingwa msimu wa Ligi Kuu Bara msimu huu,” amesema Robertinho aliyeiacha Simba katika nafasi ya pili ya msimamo na kuipa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Yanga kwa penalti katika mchezo wa fainali ya michuano hiyo iliyofanyika jijini Tanga.

SOMA NA HII  SIMBA QUEENS MGUU SAWA KUANZA KUITIKISA AFRIKA...CAF YAWABEBA KWENYE RATIBA...