Home Habari za michezo UGOMVI WA ALGERIA NA MOROCCO UPO HIVI A-Z….KUMBE WACHEZAJI WALIBADILISHIWA JEZI

UGOMVI WA ALGERIA NA MOROCCO UPO HIVI A-Z….KUMBE WACHEZAJI WALIBADILISHIWA JEZI

UGOMVI WA ALGERIA NA MOROCCO UPO HIVI A-Z....KUMBE WACHEZAJI WALIBADILISHIWA JEZI

Nakumbuka ilikuwa Januari 2022, wakati mashindano ya AFCON 2021, yanaendelea kule Cameroon.

Baada ya mchezo wa hatua ya makundi kati ya Algeria na Ivory Coast kumalizika na kupoteza kwa mabao 3-0 niliona kundi kubwa la rafiki zangu wa Morocco kwenye status za mtandao wa WhatsApp wakifurahia kipigo hicho ambacho kilisababisha Algeria iishie hatua ya makundi.

Nilipowauliza wakaniambia kwamba wao ni mahasimu wa Algeria na wanafurahia kuona wakianguka kwenye nyanja zote, hawapendi kuona Algeria hata ikishiriki achilia mbali kutolewa hatua ya makundi.

Juzi likaibuka tena suala la kuzuiwa kwa wachezaji wa RS Berkane kwenye uwanja wa ndege kisha baadaye wakaruhusiwa na walipofika uwanjani wakaambiwa watumie jezi nyingine tofauti na zile walizokwenda nazo, wakakataa, mechi ikashindikana kuchezwa na Berkane ikarudi zake Morocco.

Mwaka jana Morocco ilijiondoa katika michuano ya CHAN baada ya Algeria kugoma kuipa ndege iliyokuwa inasafirisha msafara wa timu hiyo kutoka Morocco ruhusa ya kutumia anga lao. Lakini kwanini yote haya yanatokea chanzo zaidi ni nini?

UGOMVI ULIPOANZIA

Stori baina ya timu hizi mbili inaanzia mwaka 1830 wakati ambao Ufalme wa Morocco ulikuwa una nguvu sana, kipindi hicho ukoloni ulikuwa ndio unaingia Afrika ya Kaskazini na Wafaransa walikuwa wanataka kuitawala Algeria.

Vita ikazuka baina yao na makabila ya Algeria yaliyokuwepo kwa wakati huo. Morocco ikawa inasapoti makabila hayo kupambana na Ufaransa ili wasije kutawaliwa.

Vita ikawa inaingia ugumu sana kwa Ufaransa ambao mwaka 1944, ili kushinda wakaamua kuvamia na kuua raia wa Morocco katika Mji wa Tanger ambao upo Pwana, pia ikaanzisha vita ya Battle of Isly iliyopigwa kwenye Mji wa Oujda ambao ni kilomita kadhaa kutoka Casablanca.

Baada ya hapo Morocco ikasalimu amri na kukata kabisa misaada waliyokuwa wanaitoa kwa wa Algeria. Ufaransa ikafanikisha azma yake ya kutawala.

Moja kati ya ufalme wa Morocco ilikuwa inayaogopa ilikuwa ni kama Ufaransa itatawala Algeria basi ingehamia na kwao pia. Lakini baada ya kuacha kutoa misaada kwa Algeria, Ufaransa ikaingia nao makubaliano maalumu ya kutovuka mipaka na waishie Algeria huko huko.

Miaka ikaenda na baadaye Morocco ikatawaliwa na Hispania na Ufaransa ambapo wote waligawana maeneo lakini mipaka ya Algeria na Morocco ikaendelea kuwa vilevile.

Baada ya Morocco kupata uhuru wake mwaka 1958, mfalme wao kwa wakati huo Mohamed wa tano alikuwa akisaidia sana makundi la wapigania uhuru wa Algeria (FLN), silaha, pesa na dawa ili washinde vita yao na kupata uhuru kutoka kwa wakoloni wa Ufaransa.

Ukiondoa msaada huo, pia mfalme huyo aliruhusu kundi hilo kuitumia nchi yake kama sehemu ya mafunzo ya askari wao.

Mwaka 1962, Ufaransa ilishindwa na kuipa Algeria uhuru wao, hapa ndio shida ilipoanza. Baada ya uhuru, Morocco ikaja na kile kilichoitwa Greater Morocco ambapo baadhi ya wanasiasa walidai kwamba sehemu ya Algeria, Mali, Maurtania na Jangwa la Sahara zilikuwa ndani ya Morocco.

Hapa ikazuka vita iliyoitwa ‘Sand War’ ambayo ilipigwa baina ya Morocco na Algeria mwaka 1963 na hiyo ilichagizwa hasa na kitendo cha Morocco kusema hadi Mji wa Tindouf uliopo ndani ya Algeria kwamba ni wao.

Vita ikapigwa kwa miezi miwili na baada ya hapo Oktoba 29 na 30, 1963 viongozi wa nchi hizo mbili walikutana Bamako, Mali ambapo walikubaliana kusitisha vita na mipaka ile ya wakati wa ukoloni ndio ibakie vilevile na waliopewa kazi ya kusimamia mipaka hiyo walikuwa ni wa Ethopia na Mali. Lakini hii ni kama haikufanya kazi.

Morocco ilikubali lakini ilitaka kuendelea kuvishikilia vijiji vya Hassi-Beida na Tindjoub ambako iliendelea kubakisha majeshi yake licha ya kufanya makubaliano ya kusitisha vita.

Vijiji hivyo vilikuwa ndani ya Algeria kwa mujibu wa mipaka waliyokubaliana lakini Morocco ikaendelea kusimama na kuvitaka.

Rais wa Algeria kwa wakati huo Ben Bella, akaitaka Morocco mara moja iondoe majeshi yake kwenye vijiji hivyo, wakapinga. Algeria ikaanzisha tena vita ambapo ilivamia eneo la Figuig lililokuwa ndani ya Morocco.

Walipigana kwa muda na Febuari 1964, Morocco iliondoa majeshi yake kwenye vijiji hivyo na Algeria nao wakaondoa majeshi yao Figuig, ikawa mwisho wa Sand War.

Ilipofika mwaka 1969, nchi hizi mbili zikasaini mkataba uliotwa Irfan Treay ambao ulikuwa na lengo la kumaliza tofauti zao za mipaka na kuboresha uhusiano wao, mkataba huu ulisainiwa na wawakilishi wa Mfalme Hassan wa Morocco na upande wa Algeria alikuwa rais wao Houari Boumediene.

Baada ya kusaini mkataba huu, mambo yalitulia hadi ilipofika mwaka 1975 ambapo Hispania ilitangaza kwamba inataka kuliachia eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Eneo hilo lilikuwa linapiganiwa na wana harakati wa Polisario Front ambao walikuwa wakidai uhuru wao ili waanzishe taifa lao. Katika harakati hizo Algeria ilikuwa ikiwasapoti.
Hispania ilipokubali kuliachia,

haikutangaza kwamba inaliachia eneo hilo kama taifa huru na badala yake ikaligawa nusu kwa Morocco na Maurtania.

Hilo likapingwa sana na Umoja wa Mataifa ambao walidai hakukuwa na ushahidi wowote kwamba mataifa hayo mawili yalikuwa yanastahili kuchukua maeneo hayo kwani haikuwa inajulikana kama ni ya kwao.

Wakati Hispania inagawa eneo hilo kwa Morocco na Maurtania mwaka 1975, kundi la Polisario Front lililokuwa linapigania uhuru wa eneo hilo tangu mwaka 1973 likatangaza kwamba eneo hilo ni nchi huru na wakalibatiza jina la Sahrawi Arab Democratic Republic (SADR). Algeria ikaitambua kama ni nchi rasmi mwaka mmoja baadaye na baada ya hapo ikawa inaisaidia vyakula, maji na silaha.

Ilipofika mwaka 1979, Maurtania ilitangaza kwamba haihitaji tena kushikilia eneo Sahara walilopewa na Hispania, hivyo wakaliachia. Muda mfupi tu baada ya kuliachia Morocco ikapeleka majeshi yake kwenye eneo hilo na kulichukua.

Vita kali iliendelea baina ya Morocco na wapigania uhuru wa Sarhawi hadi ilipofika pale eneo hilo lilipopewa uachama na Umoja wa Afrika (OAU) kwamba ni nchi huru.

Kuanzia hapo presha ikazuka sana kwa Morocco kutoka mataifa mbalimbali duniani wakiwataka waliachie eneo hilo.

Serikali ya Morocco ikaona isiwe tabu mwaka 1981 ikatangaza kwamba italiachia eneo hilo kwa makubaliano maalumu ambayo yalitakiwa kupitishwa na Umoja wa Afrika, lakini haikupitishwa katika kura za maoni.

Ilipofika mwaka 1987, Morocco ilitangaza kuitambua Polisario (kundi linalopambania uhuru wa Sarhawi), kisha wakakubali kumaliza tofauti zao na Algeria ingawa hakukuwa na maandishi yoyote kama mkataba, ilikuwa ni kwa njia ya mdomo tu.

Mambo yakatulia na ilipofika mwaka 1996 likaibuka jingine. Morocco iliilaumu idara ya usalama wa taifa ya Algeria kwamba imehusika katika shambulio la bomu katika Jiji la Marakech ambako Wahispania wawili waliuawa.

Kwa sababu hiyo, Morocco ikaweka sharti la Visa kwa raia yoyote wa Algeria ambaye angetaka kutembelea kwao.

Algeria wao wakajibu mapigo kwa kufunga mipaka yao jambo ambalo linapoteza walau asilimia mbili ya pato la taifa kwa nchi hizo mbili kila moja.

Mwaka 1999, rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika alihudhuria mazishi ya mfalme wa Morocco Hassan na akatangaza siku tatu za maombolezo kwa raia wa Algeria jambo lililoonekana kuleta matumaini.

Lakini baada tu ya kuondoka nchini humo na kurudi Algeria, alisema Morocco inasapoti kundi la kigaidi la GIA ambalo linapambana na serikali yao, pia akaishtumu Morocco kuwa inaingiza dawa za kulevya Algeria, mambo yakaharibika na uhasama ukarudi upya.

Julai 2004, mfalme wa Morocco Mohammed VI alifuta sharti la Viza kwa raia wa Algeria.

Nchi hizi ziliendelea kuwa na uhusiano mbovu ambapo Algeria imekuwa ikiishtumu Morocco kuwa inasapoti makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati za kutaka kuipindua serikali yao.

Mwaka 2021, mamlaka za Algeria ziliripoti kwamba Morocco inashirikiana na Israel kufuatilia mawasiliano ya raia 6000 wa nchi hiyo na wakiwemo viongozi wao wa juu.

Agosti mwaka huo huo, Algeria ikaishtumu tena Morocco kwamba inalisaidia kundi la MAK ambalo linapambana kutaka eneo la Kablye lililopo ndani ya Algeria liwe huru.

Morocco ikajibu shutuma hizi kwa kuitaka Algeria ikubali iwasaidie kupamabana na kundi hilo, Algeria haikujibu na badala yake mwezi huo waziri wa mambo ya nje wa Algeria, Ramtane Lamamra akatangaza kwamba wamevunja uhusiano wa kidiplomasia na Morocco, hiyo ikasababisha Morocco ifunge ubalozi wake ndani ya Algeria.

Ilipofika Septemba 22, 2021 Algeria ikafunga anga lake kuzuia ndege yoyote ya Morocco kupita. Haijalishi Iwe imebeba wanajeshi ama raia wa kawaida.

Lakini ilipofika mwaka Septemba 08, 2023 Algeria iliachia anga lake kutumiwa na Morocco, ingawa hadi sasa wameendelea kutokuwa na maelewano mazuri, kila uchao limekuwa likiibuka jipya.

Kwa sasa ugomvi zaidi ni kuhusu Sarhawi ambayo bado Morocco ameendelea kuishikilia, lakini pia migogoro ya Algeria kuishtumu Morocco inasapoti magaidi wanaowashambulia na Morocco inawashtumu Algeria kwa masuala ya kigaidi yanayotokea nchini mwao.

Kufikia hapa unaweza kupata picha kwanini Algeria ilikataa jezi ya Berkane zilizokuwa zina ramani ya Morocco iliyojumuisha eneo la Sarhawi kwa sababu Algeria wao wanaitambua kama nchi huru wakati Morocco wanatambua kama ni sehemu yao.

SOMA NA HII  SIRI HII YAVUJA...KUMBE DUBE NDIO SABABU...AZAM KUFUNGWA NA SIMBA