“Nilikuwa nikicheza na kaka zangu kama Haruna Moshi ‘Boban’, Amri Kiemba, na wenzangu wengine Seseme na Salum Abubakar ‘Sure Boy’. Nilikuwa nanaf urahia, kwani ni mafundi, ila wapo wengi; kwa kifupi hao ni baadhi,” anasisitiza, akisema aliyekuwa anamkubali tangu akiwa mtoto ni Boban.Anasema vitu ambavyo hatakaa avisahau ni kupandishwa kutoka timu B kwenda Simba A. Uchungu alioupata ni kukosa mishahara ya miezi mitatu: “Baada ya kupanda, nikatamani niachane na soka. Kaka zangu walisema napaswa kuongeza bidii nitaanza kufurahia kipaji changu, na maneno yao yalitimia baada ya kuyazingatia. Jambo lingine nilipata nafasi ya kuitumikia Taifa Stars.”
Anasema nje ya mpira wa miguu anapendelea kusoma vitabu vyenye mafunzo, akikitaja kimojawapo kuwa ni Watoto wa Mama Ntilie, kilichojaa mafunzo ya kweli ya mtaani.
“Watu tulikotokea maisha ya chini, hicho kitabu ukikisoma kina funzo, tofauti na watoto wa ushuani. Napenda kusoma vitabu mbalimbali ili kupanua uwezo wa kufikiri na kutafsiri vitu katika jamii,” anasema.
Singano anakumbuka akiwa mdogo alikuwa akienda na wenzake majalalani kuokota mkaa; kisha akiukusanya mwingi anapeleka nyumbani. Wakati mwingine anauza ili kupata fedha ya kujikimu au kumpa mama yake mzazi kusaidia nyumbani.
“Tunaenda ambako gari la mkaa limeshuka, tunaokota uliobaki; wakati mwingine mpaka majalalani. Kifupi, nimepitia mengi, lakini nashukuru Mungu hapa nilipo sasa haikuwa rahisi hadi Watanzania kunifahamu. Jambo ninalolitamani ni wazazi wangu wangekuwa hai, wangekula kidogo nilichokipata,” anasema Singano, akiwa mtoto wa mwisho kati ya sita; kaka zake wakiwa ni Khamis, Moghammed na Bakari, huku wawili wakitangulia mbele ya haki.