Habari za Yanga leo
Yanga SC

ZA NDAAANIII KABISAAA…..MASTAA HAWA 6 ‘HAWANA CHAO’ NDANI YA YANGA LIGI IKIISHA…

admin May 15, 2026 6:30 pm

WAKATI vita ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa Yanga ikiendelea, vigogo wa klabu hiyo wako kwenye hesabu kali za kukiboresha kikosi hicho, huku panga kali likiendelea kunolewa kwa ajili ya mastaa wa kigeni sita.

Iko hivi; kuna mastaa ambao Yanga iliwasajli msimu huu lakini changamoto kubwa ni kwamba, wachezaji hao wameshindwa kukamilisha mipango ya kuongeza nguvu kikosini hali iliyofanya baadhi yao kutolewa kwa mkopo na wengine kusotea benchi.

Katika orodha ambayo inasemekana iko kwenye mikono ya mabosi wa Jangwani, kuna winga Buba Jammeh ambaye alijiunga na Yanga kupitia usajili wa dirisha dogo Januari 2026 akisaini mkataba wa miaka miwili, amecheza mechi kumi za Ligi Kuu Bara akiwa na asisti moja ambapo usajili wake ulifanywa na kocha Pedro Goncalves aliyeondolewa Mei 6, 2026.

Taarifa za ndani kutoka Yanga zilisema  kuwa: “Usajili wa Buba umechangia kwa kiasi fulani kukatishwa kwa mkataba wa Goncalves kutokana na mabosi kutumia gharama kubwa kumsajili, lakini uwezo wake ukashindwa kuiongezea kitu timu.”

Mbali na winga huyo, kiungo Lassine Kouma ambaye alitua Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Stade Malien ya Mali na kusaini mkataba wa miaka miwili, naye yupo kwenye kikaango hicho.

Licha ya kiungo huyo raia wa Chad kufunga bao moja kwenye ligi katika mchezo wa kwanza dhidi ya Pamba Jiji, lakini namba zake zimeshindwa kuwashawishi waajiri wake kutokana na kucheza mechi kumi pekee za ligi kati ya 22 kabla ya kikosi hicho kukabiliana na Dodoma Jiji.

Mwingine ni beki Frank Assinki ambaye anacheza hapo kwa mkopo wa msimu mzima akitokea Singida Black Stars akiwa ametumika kwenye mechi tisa za ligi.

Licha ya kwamba amekuwa akifanya vizuri kila anapopewa nafasi, lakini hesabu za mabosi wa Yanga ni kwamba hawataendelea naye huku nafasi yake akitafutwa mzawa.

Mbali na mastaa hao ambao wameendelea kuwepo kikosini lakini muda mwingi wanasugua benchi, pia Yanga ina mpango wa kuchana na viungo Mohamed Doumbia, Celestin Ecua na Moussa Balla Conte ambao wote wametolewa kwa mkopo wakati wa usajili wa dirisha dogo msimu huu.

Ecua raia wa Chad ambaye yupo JS Kabylie ya Algeria, alitua Yanga akiwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu uliopita wakati anaitumikia Zoman kwa mkopo akiwa mchezaji wa ASEC Mimosas.

Kwa kipindi cha miezi sita alichocheza Yanga kabla ya kutolewa kwa mkopo, kiungo huyo aliyesaini mkataba wa miaka mitatu, alifunga bao moja, huku pia akifunga lingine huko Algeria na asisti moja.

Conte raia wa Guinea, hivi sasa anaitumikia Raja Athletic ya Morocco kwa mkopo ambapo ameendelea kusotea benchi na wakati mwingine jukwaani akipewa mechi mbili pekee chini ya kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids.

Doumbia kutoka Ivory Coast aliyesaini mkataba wa miaka miwili, naye bado hali yake ni tete huko Marumo Gallants ya Afrika Kusini ambapo Yanga inaona ni wakati muafaka wa viungo hao kuondolewa moja kwa moja, huku klabu wanazozitumikia kwa sasa zikitaka kutoa tathmini zao kama zitahitaji kubaki nao au la. Kiungo huyo amecheza mechi saba za Ligi Kuu ya Afrika Kusini akifunga bao moja.

Kiongozi mmoja kutoka Yanga, alisema kuwa, timu hiyo inataka kusahihisha kwa kufanya usajili mkubwa kuelekea msimu ujao ambapo tayari msako wa mastaa wapya umeshaanza kimya kimya.

“Tunajua tulipojikwaa, sio kwamba tulipata wachezaji wabovu lakini kiukweli walikuwa wana namba nzuri kabla, walipokuja hapa wakashindwa kutupa kile tulichokitarajia, tutafanya usajili mkubwa sana,” alisema kiongozi huyo.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, aliwahi kusema kuwa: “Tunafuatilia kwa ukaribu maendeleo ya hao wachezaji. Watathmini wetu wa video wanawafuatilia kuangalia viwango vyao ambapo kwa mechi ambazo wanacheza tumekuwa tukitazama na iwapo na sisi tunakuwa na mechi, huwa mechi zao zinarekodiwa kisha benchi la ufundi linakuja kuwatazama baadaye. Tumekuwa tukiwasiliana na hizo timu kupata viwango vya utimamu ili kupata maendeleo yao.

“Baada ya msimu kumalizika, benchi la ufundi ndio litatoa tathmini ya jumla juu ya nafasi ya kila mmoja kama anarudishwa au la.”

KUHUSU UWANJA MPYA WA YANGA…HAYA HAPA YANAYOMPA SIFA MBADALA GSM… MHHHH…HII YA CHAMA NA OKELLO NI SAWA NA PIGA NIKUPIGE….