IKIWA imesalia siku moja kuelekea mechi ya watani wa jadi kati ya Simba na Yanga, Kocha mkuu wa Simba pamoja na kipa wa timu hiyo wameahidi kupata ushindi katika mchezo huo.
Kocha Didier Gomes na kipa Aishi Manula wamezungumza jioni ya leo baada ya kumalizika kwa mazoezi kwenye uwanja wao wa Mo Simba Arena na kutamba kushinda mechi ya Jumamosi .
“Timejipanga vizuri kama wachezaji kuhakika tunawapa mashabiki zetu furaha kwa kutwaa ubingwa tukishinda mbele ya Yanga”amesema Manula na kuongeza:
“Tuna timu bora ambayo inaweza kukabiliana na timu yoyote hivyo niseme tu tupo tayari kwa mapambano na kushinda,” amesema.
Naye kocha Gomes amesema wamejipanga vizuri kutoa urudani na kushinda mchezo huo ambao kimsingi kama Simba SC wakishinda wanakuwa mabingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya nne mfululizo.
“Tumejipanga vizuri na lengo ni kutwaa ubingwa ambao kwa asilimia kubwa tunakaribia kuupata.
Ni mara ya kwanza kwenye ligi nakutana na kocha wa Yanga Nabi, namuheshimu ila lengo letu ni kuibuka na ushindi katika mchezo huo muhimu hivyo lazima tufanye hivyo,” amesema Gomes.
Kwa mara ya mwisho timu hizi zilipokutana kwenye ligi, mechi ilimalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1.