SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limekiri kupokea barua ya kutaka kujiuzulu kwa nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta ‘Samagol’, lakini imemkaushia kwamba hadi watakapofanya kikao cha pamoja ili kujadiliana naye.
Kabla ya TFF, kutoa msimamo huo, Gazeti la Mwanaspoti liliandika mapema wiki iliyopita kuhusiana na hatua ya Samatta kuandika barua, ambapo baba mzazi wa supastaa huyo, Ally Pazi Samatta alilifafanua jambo hilo.
“Japo Mbwana hakuniambia chochote kuhusiana na uamuzi wake, nililetewa barua kutoka kwa mtu ambaye siwezi kumtaja jina, nimeisoma, pamoja na yale aliyoandika sikubaliani na hilo, alitumikie taifa lake kwa ajili ya wale ambao wanamuunga mkono, changamoto haziwezi kukosekana,” alisema Mzee Samatta.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, alifafanua juu ya jambo hilo juzi akisema kwamba hawapo tayari kumuona Samatta anajiuzulu kuitumikia timu ya taifa na wamepanga kukutana naye kwanza ili wazungumze.
“Huwezi kumuacha mchezaji mwenye CV kubwa kama yake, anajiuzulu kirahisi, sisi kama viongozi wa TFF, hatupo tayari kwa hilo, tutakaa chini kuzungumza naye,” alisema Kidao na kuongeza;
“Samatta alikuwa mchezaji bora wa Afrika akiwa TP Mazembe, alichukua ubingwa akiwa na KRC Genk, pia juzi kachukua ubingwa akiwa na Paok ya Ugiriki, mbali na kuwa mchezaji wa kwanza Mtanzania kucheza Ligi Kuu ya England aliposajiliwa Aston Villa, kafanya vitu vingi vya kuiheshimisha nchi, hilo kama viongozi hatuwezi kulichukulia kirahisi,” alisema Kidao.
Alisema Samatta ameifanyia mengi sana nchi hii katika soka na si rahisi kwa TFF kukubali moja kwa moja.
“Kwanza ni nahodha wa timu wa timu ya taifa, Taifa Stars na ameiongoza vizuri sana katika mafanikio ya sasa. Ameongoza Taifa Stars kufuzu mara mbili fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 na 2023, mbali na fainali ya CHAN 2022 pia amekuwa kiongozi mzuri wa wachezaji katika michuano ya Afcon iliyopita pamoja na kutofuzu hatua ya mtoano,” alisema Kidao.
Alifafanua Samatta pia ni mchezaji wa kwanza wa Kitanzania kucheza michuano yote mikubwa ya Ulaya ambayo ni Ligi ya Mabingwa, Europa League na Europa Conference League.
Mbali ya michuano hiyo, katika maisha yake ya uchezaji wa kulipwa Ulaya nahodha huyo wa Taifa Stars, ametwaa mataji mawili ya ligi akiwa na KRC Genk ya Ubelgiji msimu wa 2018/19 na PAOK msimu uliomalizika huko Ugiriki.
Pia ana medali aliyopata msimu wa 2019/20 katika fainali ya Kombe la Carabao England akiwa na Aston Villa baada ya kupoteza mbele ya Manchester City kwenye Uwanja wa Wembleyn kwa mabao 2-1, bao la Villa lilifungwa na mshambuliaji huyo.
Kabla ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, Samatta alizichezea Mbagala Market, African Lyon na Simba.