Home news BAADA YA MECHI 10…HIVI NDIVYO FADLU ANAVYOPITA KWENYE NJIA YA SVEN NA...

BAADA YA MECHI 10…HIVI NDIVYO FADLU ANAVYOPITA KWENYE NJIA YA SVEN NA GOMEZ….

Habari Simba

KOCHA mkuu wa Simba, Fadlu Davids amefikisha jumla ya michezo 10 ya Ligi Kuu Bara tangu alipoanza kukinoa rasmi kikosi hicho Julai 5, mwaka huu akichukua nafasi ya Mualgeria, Abdelhak Benchikha aliyeondoka Aprili 28, 2024.

Fadlu, raia wa Afrika Kusini, ameanza ligi vyema tangu atoke kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Morocco timu ya Raja Casablanca akiwa ni msaidizi wa Josef Zinnbauer. Kupitia yeye, hapa kuna makocha waliopita Simba na walichokifanya katika michezo 10 ya mwanzoni katika ligi tangu 2019.

SVEN VANDENBROECK

Baada ya Simba kuachana na Patrick Aussems, ilimpa kazi Mbelgiji mwenzake, Sven ambaye alianza kwa kushinda mataji matatu ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) msimu wa 2019-2020, pia Ngao ya Jamii mwaka 2020.

Sven alianza kazi Simba Desemba 12, 2019 na katika michezo yake 10 ya mwanzoni alishinda minane, sare mmoja na kupoteza mmoja.

Michezo aliyoshinda ni dhidi ya Lipuli (4-0), KMC (0-2), Ndanda (2-0), Mbao (2-1), Alliance (4-1), Namungo (3-2), Coastal Union (2-0) na Polisi Tanzania (2-1) huku sare ikiwa ni dhidi ya Yanga (2-2) na kichapo kutoka kwa JKT Tanzania cha bao 1-0.

Katika michezo hiyo, Sven alikusanya pointi 25, huku timu ikifunga mabao 23 na kuruhusu manane.

DIDIER GOMES

Mfaransa huyu alijiunga na Simba Januari 24, 2021 akichukua nafasi ya Sven ambaye kipindi hicho alienda kujiunga na FAR Rabat ya Morocco.

Katika michezo yake 10 ya mwanzo, Gomes alishinda minane na kutoka sare miwili ambapo ya ushindi ni dhidi ya Dodoma Jiji (2-1), Biashara United (1-0), JKT Tanzania (3-0), Mtibwa Sugar (5-0), Mwadui (1-0), Kagera Sugar (2-0), Gwambina (1-0) na Dodoma Jiji (3-1), huku ile miwili ya sare ni dhidi ya Azam (2-2) na Tanzania Prisons (1-1).

Gomes alivuna pointi 26 katika michezo hiyo na timu ikifunga mabao 21, ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano.

PABLO FRANCO

Raia huyo wa Hispania alitambulishwa Simba Novemba 8, 2021 akitokea klabu ya Ligi Kuu ya Kuwait ya Al-Qadsia akichukua nafasi ya Gomes aliyeondoka baada ya kutolewa raundi ya kwanza tu ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Katika michezo 10 ya mwanzo ya Ligi Kuu Bara, Pablo alishinda sita, sare miwili na kupoteza pia miwili huku ya ushindi ni (3-1) v Ruvu Shooting, (2-1) v Geita Gold, (4-1) v KMC, (2-1) v Azam FC, (1-0) v Tanzania Prisons na (1-0) v Mbeya Kwanza.

Michezo ya sare ni (0-0) v Yanga, (0-0) v Mtibwa Sugar huku ile ya kichapo ni (1-0) v Mbeya City na (1-0) v Kagera Sugar ambapo Pablo alikusanya pointi 20 na katika mechi hizo alifunga jumla ya mabao 13 tu na nyavu zake kutikiswa mara sita.

ZORAN MANOJLOVIC MAKI

Kocha huyo mwenye uraia pacha wa Serbia na Ureno alijiunga na Simba Juni 28, 2022 ingawa aliondoka Septemba 6, 2022 kwa kile kilichoelezwa na aliyekuwa ofisa mtendaji mkuu wa kikosi hicho, Barbara Gonzalez kufikia makubaliano ya pande mbili.

Katika kipindi chake cha uongozi, Zoran aliiongoza Simba katika michezo miwili ya Ligi Kuu Bara na kushinda yote akianza na ushindi wa (3-0) v Geita Gold, (2-0) v Kagera Sugar huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao matano bila ya kuruhusu.

JUMA MGUNDA

Baada ya kuondoka Zoran, Simba ilimtangaza aliyekuwa kocha mkuu wa Coastal Union kwa wakati huo, Juma Mgunda Septemba 7, 2022, ingawa kwa sasa anaifundisha Namungo na katika michezo 10 ya mwanzo alishinda sita, sare mitatu na kupoteza mmoja.

Michezo ya ushindi ni (1-0) v Tanzania Prisons, (3-0) v Dodoma Jiji, (5-0) v Mtibwa Sugar, (1-0) v Ihefu SC, (1-0) v Namungo FC na (4-0) v Ruvu Shooting huku ya sare ni (1-1) v Yanga, (1-1) v Singida Fountain Gate na (1-1) v Mbeya City.

Mechi aliyopoteza ni (1-0) v Azam FC ambapo Mgunda katika michezo hiyo 10 alikusanya jumla ya pointi 21, ambapo safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho kwa wakati alichokiongoza kilifunga mabao 18, huku eneo lake la ulinzi likiruhusu manne tu.

ROBERTO OLIVEIRA ‘ROBERTINHO’

Januari 3, 2023 uongozi wa Simba ulimtambulisha Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kuwa kocha mpya kwa mkataba wa miaka miwili.

Katika michezo 10 alishinda minane na kutoka sare miwili ambapo ya ushindi ni (3-2) v Mbeya City, (1-0) v Dodoma Jiji, (3-1) v Fountain Gate, (3-0) v Mtibwa Sugar, (2-0) v Ihefu SC, (2-0) v Yanga, (3-0) v Ruvu Shooting na (6-1) v Polisi Tanzania.

Sare ni (1-1) v Azam FC na (1-1) v Namungo FC ambapo ‘Robertinho’ katika utawala wake alivuna pointi 26, katika michezo 10 ya mwanzo, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 25 na eneo la ulinzi likiruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita.

ABDELHAK BENCHIKHA

Benchikha alijiunga na kikosi hicho Novemba 24, 2023 akitoka kuipa USM Alger ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuifunga Yanga kwa faida ya bao la ugenini kufuatia sare ya 2-2 na CAF Super Cup mbele ya Al Ahly ya Misri.

Kocha huyo katika michezo yake ya kwanza alishinda saba, sare miwili na kupoteza mmoja ambapo ile ya ushindi ni (3-0) v Kagera Sugar, (1-0) v Mashujaa FC, (4-0) v Tabora United, (1-0) v Geita Gold, (1-0) v JKT Tanzania na (2-1) v Coastal Union.

Mingine ni (3-1) v Fountain Gate huku ile ya sare ni (2-2) v KMC, (1-1) v Azam FC na ya kichapo ni cha (2-1) v Tanzania Prisons ambapo Benchikha alikusanya jumla ya pointi zake 23, katika michezo yake 10, akifunga mabao 19 na kuruhusu saba.

FADLU HUYU HAPA

Kwa sasa kikosi cha Simba kinanolewa na Fadlu Davids ambaye alijiunga nacho Julai 5, mwaka na katika michezo yake 10 ya mwanzo tayari ameshinda minane, sare mmoja na kupoteza pia mmoja ambapo amekusanya jumla ya pointi 25, akiwa kileleni.

Michezo ya ushindi ni ile ya (3-0) v Tabora United, (4-0) v Fountain Gate, (2-0) v Azam FC, (1-0) v Dodoma Jiji, (1-0) v Tanzania Prisons, (3-0) v Namungo FC, (1-0) v Mashujaa na (4-0) v KMC FC, huku mchezo wa sare ni (2-2) v Coastal Union.

Kichapo kwa Fadlu ni cha bao 1-0 dhidi ya Yanga huku safu ya ushambuliaji ikiwa imefunga jumla ya mabao 21 na kuruhusu matatu.

Tangu 2019, makocha wa Simba waliovuna pointi nyingi katika michezo yao 10 ya mwanzo ya Ligi Kuu Bara ni Didier Gomes Da Rosa na Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambao wamekusanya 26, wakifuatiwa na Sven Vandenbroeck na Fadlu wenye 25.

Wanaofuatia ni Abdelhak Benchikha aliyekusanya pointi 23, huku Juma Mgunda akiwa na 21 wakati Pablo Franco alikusanya 20 tu.

KAULI YA FADLU

Akizungumzia mwenendo wake katika Ligi Kuu Bara, Fadlu Davids anasema wako kwenye mwelekeo mzuri ingawa bado wana kazi kubwa ya kufanya kuendelea kukaa kileleni, huku akiweka wazi siri ya mwanzo mzuri ni kutokana na ushirikiano anaoupata.

“Muda mwingine tunakosa mwendelezo mzuri kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo kushindwa kutumia vizuri nafasi za kufunga tunazozipata, ingawa nashukuru tumeendeleza umoja wetu ambao ndio siri na chachu ya kufikia hapa tulipo sasa.”

Msimamo wa mechi 10 za mwanzo za makocha wapya Simba tangu 2019:

                                      P W D L F A PTS

Roberto Oliveira              10 8 2 0 25 6 26

Didier Gomes Da Rosa    10 8 2 0 21 5 26

Fadlu Davids                   10 8 1 1 21 3 25

Sven Vandenbroeck         10 8 1 1 23 8 25

Abdelhak Benchikha        10 7 2 1 19 7 23

Juma Mgunda                 10 6 3 1 18 4 21

Pablo Franco                  10 6 2 2 13 6 20

Credit:- Mwanaspoti

SOMA NA HII  MAANDALIZI MUHIMU KUELEKEA MSIMU MPYA