Home Habari za michezo HIZI HAPA DK 90 ZA JASHO NA DAMU ZILIVYOIPUNGUZA KASI YANGA KLABU...

HIZI HAPA DK 90 ZA JASHO NA DAMU ZILIVYOIPUNGUZA KASI YANGA KLABU BINGWA AFRIKA…

Habari za Yanga leo

BAO la dakika za jioni lililowekwa kimiani na mshambuliaji aliyetokea benchi, Prince Dube imeiokoa Yanga isife ugenini jijini Lubumbashi, DR Congo baada ya kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya wenyeji TP Mazembe na kufufua kwa mbali tumaini la kutakati tiketi ya robo fainali kama itazitumia vyema mechi tatu ilizosaliwa nazo.

Ikicheza kwenye Uwanja wa Mazembe, Yanga ilisubiri hadi dakika tano za nyongeza za mchezo huo, baada ya Dube kutumbukiza mpira wavuni na wa kunyong’onyesha wenyeji walioenda mapumziko wakiwa na bao moja lililofungwa dakika ya 41 na Cheikh Fofana aliyekuwa ana dakika tatu uwanjani tangu aingie uwanjani.

Fofana aliingia dakika ya 39 kuchukua nafasi ya Gloire Mujaya aliyeumia na alipiga krosi dogo iliyoenda kugonga mlingoti wa lango la Yanga lililokuwa likilindwa na kipa Gjigui Diarra na kudumbukia wavuni licha ya Ibrahim Bacca kujaribu kuokoa kwani mwamuzi Ibrahim Kalilou Troure wa Ivory Coast alishawaita kati.

Katika mchezo huo uliomaliza jioni hii, Yanga ilicheza kichovu kipindi cha kwanza licha ya kocha Sead Ramovic kuwaanzisha Kiungo Khalid Aucho na Dickson Job waliokosa mchezo uliopita dhidi ya MC Alger.

Kabla ya sare ya jana, Yanga ilishapoteza mechi mbili za kundi hilo ikifungwa 2-0 nyumbani na ugenini na Al Hilal ya Sudan na MC Alger ya Algeria mtawalia na sasa imesaliwa na michezo mitatu ya kuamua hatma yake katika kundi hilo linaloongozwa na Wasudan watakaoikaribisha MC Alger kuanzia saa 4 usiku wa leo.

Lile soka tamu la kushambulia kwa kasi na kukaba kuanzia juu, ni kama limepotea kwa Vijana wa Jangwani tangu kocha Sead Ramovic kuchukua mikoba ya Miguel Gamondi aliyefurushwa hivi karibuni baada ya Yanga kupoteza mechi mbili za Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam (1-0) na Tabora United waliowafunga 3-1.

Katika mchezo wa leo Yanga ilikuwa inapoteza mipira mingi mbele ya wachezaji wa timu wenyeji, huku kipa Diarra Djigui akitumika kwa dakika 45 tu baada ya kuumia akiwa tayari ameshatunguliwa bao hilo.

Kocha Ramovic alimtoa Diarra pamoja na Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya na kuwaingiza Abubakar Khomeiny, Clement Mzize na Stephane Aziz KI kabla ya kuwatoa tena Kennedy Musonda na Duke Abuya na kuwaingiza Prince Dube na Clatous Chama ambao waliongeza kasi ya mashambulizi.

Sare hiyo ya leo licha ya kuifanya Yanga kuendelea kusalia mkiani mwa kundi hilo ikiwa na pointi moja, huku Mazembe ikifikisha mbili kila mmoja ikicheza mechi tatu, lakini haikufurahisha mashabiki wa klabu hiyo kutokana na soka inalocheza kwa sasa timu chini ya Ramovic.

Yanga itarudiana na Mazembe wiki ijayo kabla ya kumalizana na Al Hilal kabla ya kuipokea MC Alger siku ya mwisho wa mechi za makundi ambapo, wababe hao wanahitajika kushinda zote ili kufikisha pointi 10 na kufuzu robo fainali kwa mara ya pili mfululizo, baada ya msimu uliopita kufika huko chini ya Gamondi aliyetemeshwa kazi mara baada ya kuifikisha timu hiyo makundi.

Katika kipindi cha kwanza kwa mechi ya leo Mazembe ilitawala sehemu kubwa ya mchezo, huku Yanga ikitengeneza nafasi chache, huku kipa Diarra akionekana kama ameumia na kuomba kutolewa kabla ya kuachwa amalize dakika 45 na kutolewa sambamba na wenzake wawili.

Kipindi cha pili baada ya mabadiliko hayo angalau Yanga ilionyesha uhai kwa kutengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini zikawa zinapotezwa kutokana na umakini mdogo waliokuwa nao, Pacome Zouzoua na Mzize kabla ya Dube kusahihisha makosa wakati Mazembe wakisubiri filimbi ya mwisho kusherehekea ushindi wa kwanza, kwani walishapoteza mechi moja iliyopita dhidi ya Al Hilal na kuambulia sare mbele ya MC Alger.

Dube aliyekuwa hajafunga katika mechi 13 mfululizo zilizopita zikiwamo 11 za Ligi Kuu na nyingine mbili za CAF hatua hiyo ya makundi, lakini jana aliipata ‘code number’ kwa kufunga bao hilo dakika za majeruhi na kuiokoa timu hiyo ilipasuka katika mechi ya tatu mfululizo ya Kundi A, kwani ingekuwa aibu kwa klabu hiyo.

Yanga imecheza makundi ya Ligi ya Mabingwa katika msimu ya mwaka 1998, 2023-2024 na msimu huu, lakini ilishacheza pia mara tatu Kombe la Shirikisho 2016, 2018 na 2022-2023 ilipofika fainali na kulikosa taji mbele ya USM Alger kwa kanuni ya bao la ugenini kwani matokeo ya jumla yalikuwa ni 2-2, Yanga ikishinda ugenini 1-0 na kufungwa nyumbani 2-1.

Katika mara zote ilipocheza makundi ilikuwa haijawahi kupoteza mechi mfululizo, kabla ya Dube kufanya yake na kuiokoa dakika ya jioni.

Vikosi vilivyocheza leo;

MAZEMBE: Badara Faty, Johnson Atibu, Merceil Ngimbi/Abdallah Fabrice, Boubacar Hainikoye, Oscar Kabwit, Boaz Ngalamulume, Oussein Badamassi/Zemanga Soze, Gloire Mujaya/Cheikh Fofana, Ernest Luzolo, Magloire Ntwambe(c)na Sosue Mungwengi

YANGA: Diarra Djigui/Abukabar Khomeiny, Yao Kouassi, Nickson Kibabage, Ibrahim Job, Dickson Job (c), Khalid Aucho, Maxi Nzengeli/Clement Mzize, Duke Abuya/Clatous Chama, Kennedy Musonda/Prince Dube, Mudathir Yahya/Stephane Aziz KI na Pacome Zouzoua

SOMA NA HII  YANGA KIBARUANI LEO KUUSAKA UBINGWA WA AFRIKA