Uimara wa safu hiyo ya ulinzi, uliichukua Yanga hadi dakika ya 41 kuja kupiga kona ya kwanza ambayo nayo haikuwa na madhara na kuiweka TRA United salama.
Katika kipindi hicho cha kwanza, timu zote zilikuwa zikijenga mashambulizi kupitia pembeni ambapo TRA United iliwatumia zaidi mawinga wake, Joseph Akandwanaho na Ramadhan Chobwedo kuwashughulisha mabeki wa Yanga, Mohammed Hussein (kushoto) na Israel Mwenda (kulia).
Hata hivyo, Mwenda alishindwa kuendelea na mechi wakati kipindi cha pili kinaanza aliingia Yao Kouassi Attohoula kuchukua nafasi yake.
Sheikhan Ibrahim alikuwa nyota wa kwanza wa Yanga kuonyeshwa kadi ya njano dakika ya 60, baada ya kumuangusha Chobwedo.
Baada ya Kocha wa Yanga, Pedro, Goncalves kuona ana uhitaji wa bao, dakika ya 65, akafanya mabadiliko ya wachezaji wawili, waliingia Allan Okello na Mudathir Yahya, akiwatoa Sheikhan na Duke Abuya. Hata hivyo, TRA United waliendelea kuwa imara.
Ettiene Ndayiragije naye akafanya mabadiliko kwa TRA United, dakika ya 66, akamtoa Chanda Chewa na kuingia Omary Yusuph kuendeleza uimara eneo la ushambuliaji kwa kucheza sambamba na Amy Mapaka.
Dakika ya 77, TRA United ilipata pigo kufuatia kiungo wakke, Mzamiru Yassin kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na mwamuzi Nassor Mwinchui kutoka Tanga iliyofuatia na nyekundu. Hivyo TRA ikacheza pungufu kwa takribani dakika 19 kwani baada ya kufika tisini, ziliongezwa sita.
Kulikuwa na vita kubwa eneo la kati ya uwanja ambapo Mzamiru Yassin na Jamal Dulaz, walionyeshana umwamba na viungo wa Yanga, Mohamed Damaro na Duke Abuya. Mbali na vita hivyo, pia walinzi wa TRA United, Chamoue na Kombo, waliifanya kazi nzuri ya kulinda lango lao mbele ya washambuliaji wa Yanga.
Huenda baada ya mechi hii Yanga ikaongeza majeruhi kwani Dube alitolewa dakika ya 21 kwa kuumia, pia beki wa kulia, Israel Mwenda naye hakuendelea kipindi cha pili kutokana na kile cha kwanza kuumia.Suluhu hiyo imeifanya Yanga kufikisha pointi 37 ikiendelea kukaa kileleni kwa tofauti ya pointi tisa dhidi ya Azam na JKT Tanzania zinazoshika nafasi ya pili na tatu zikiwa na pointi 28, huku Simba ni ya nne na pointi 27.Hii ni mechi ya pili mfululizo Yanga inatoka uwanjani bila kufungana baada ya kupata matokeo kama hayo dhidi ya Azam, wikiendi iliyopita. Lakini pia, msimu huu Yanga katika mechi zote ilizoshindwa kupata ushindi, hakukuwa na bao.Yanga imecheza mechi 15 ikikamilisha duru la kwanza ikishinda 11 na sare nne, haijapoteza, wakati Azam imeshuka dimbani mara 14 na kesho Alhamisi itakuwa Kigoma kukabiliana na Mashujaa ikienda kuhitimisha duru la kwanza, wakati Simba ina mechi 12, kesho Alhamisi ni ya 13 dhidi ya Pamba Jiji, hivyo ikipiga vizuri hesabu zake katika mechi hizo tatu ili kuwa sawa na Yanga, itakuwa nyuma ya watani zao hao wa jadi kwa tofauti ya pointi moja pekee.