AZAM FC YATINGISHA SOKO LA USAJILI YAKARIBIA KUMALIZA DILI LA MSHAMBULIAJI HATARI
UONGOZI wa Azam FC umefikia katika hatua nzuti katika harakati zake za kuimarisha kikosi kuelekea msimu ujao baada ya kufikia makubaliano ya kibinafsi na mshambuliaji hatari wa KCCA FC, Ivan Ahimbisibwe.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani, mabosi wa Azam FC na uongozi wa KCCA FC wameingia kwenye mazungumzo ya kina ambayo sasa yamefikia hatua za mwisho, huku kinachosubiriwa kikionekana kuwa ni tangazo rasmi tu la kukamilisha dili hilo.
Ahimbisibwe ambaye amekuwa moto wa kuotea mbali katika Ligi Kuu ya Uganda, ameonyesha ubora mkubwa wa ufungaji katika misimu miwili iliyopita, hali iliyomfanya kuwa miongoni mwa washambuliaji wanaoogopwa zaidi.
Msimu wa 2024/25 alifunga mabao 16 na kumaliza akiwa mfungaji wa pili bora nyuma ya Allan Okello aliyefunga mabao 19, kabla ya msimu wa 2025/26 kuendelea kung’ara zaidi kwa kufunga mabao 14 na kutwaa kiatu cha dhahabu cha ligi hiyo.
Uimara huo wa ufungaji umeifanya Azam FC kuona ni wakati sahihi wa kuongeza nguvu kwenye safu yao ya ushambuliaji, wakiamini ujio wake unaweza kuongeza ushindani mkubwa ndani ya kikosi.
Iwapo dili hilo litakamilika rasmi,
Ahimbisibwe atakuwa miongoni mwa wachezaji wachache wa Uganda kujiunga na Ligi Kuu Tanzania Bara, jambo ambalo tayari limeanza kuzua msisimko mkubwa kwa mashabiki wa Azam FC mitandaoni.