DAVIDO KUTUMBUIZA KOMBE LA DUNIA
Mwanamuziki Davido amethibitishwa kuwa mmoja wa wasanii watakaotumbuiza katika tamasha la awali la kuelekea Kombe la Dunia la FIFA 2026, litakalofanyika Juni 10, Jijini Los Angeles, Marekani.
FIFA ilitangaza habari hiyo Jumanne kama sehemu ya shughuli za kuelekea kuanza kwa Kombe la Dunia linalofanyika Marekani, Canada na Mexico.
Kwa mujibu wa FIFA, Davido atapanda jukwaani pamoja na Major Lazer, tamasha hilo litaoongozwa na DJ na mtayarishaji wa muziki kutoka Marekani, Diplo, katika sehemu ya tamasha itakayofanyika Los Angeles.
Tamasha hilo ni sehemu ya programu ya burudani ya moja kwa moja itakayounganisha mashabiki katika nchi zote tatu wenyeji kupitia muziki, soka na maonesho ya kitamaduni kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.
Katika taarifa yake, FIFA ilisema:“Los Angeles itakuwa mwenyeji wa sherehe za awali za tamasha kubwa, ikiwashirikisha Major Lazer wa Diplo na Davido, ambao ni wasanii wa kwanza kutangazwa kwa usiku unaotarajiwa kuwa wa kipekee wa muziki, soka na utamaduni.”
Tamasha hilo litafanyika katika ukumbi wa Crypto.com Arena, ambapo milango itafunguliwa saa 11 jioni kwa saa za Los Angeles, huku maonesho ya moja kwa moja yakitarajiwa kuanza saa moja baadaye.
FIFA imeeleza kuwa maonesho kutoka Los Angeles yataunganishwa na matukio mengine yatakayofanyika kwa wakati mmoja katika miji ya Toronto na Mexico City, na hivyo kuunda sherehe ya kipekee inayovuka mipaka ya nchi hizo tatu kabla ya mashindano kuanza.
Afisa Mkuu wa Mashindano ya Kombe la Dunia 2026 nchini Marekani, Manolo Zubiria, alisema tamasha hilo linaakisi umoja na utofauti wa tamaduni unaohusishwa na Kombe la Dunia.
Alisema: “Mfululizo wa Tamasha hayo ni shauku, umoja na mahusiano ya kitamaduni kati ya nchi tatu na dunia nzima ambayo yatakaribisha kuanza kwa Kombe la Dunia la FIFA 2026.”
FIFA pia ilitangaza kuwa tiketi za tamasha hilo zilianza kuuzwa tarehe 3 Juni, na kwamba tukio hilo litarushwa moja kwa moja duniani kote kupitia majukwaa yake ya kidijitali, ikiwemo akaunti rasmi ya Kombe la Dunia ya TikTok.
Mashabiki watakaokosa matangazo ya moja kwa moja wataweza kutazama tamasha zima pamoja na maudhui maalum ya nyuma ya pazia kupitia jukwaa la video la FIFA, VuMe Live, siku inayofuata.