Simba SC

MAGORI AFUNGUA SIRI YA UWANJA WA SIMBA BILIONI 1 KILA MWAKA ZATENGWA

Vardo June 6, 2026 5:41 pm

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, Crescentius Magori, amesema mzabuni wa jezi za klabu hiyo, Jayrutty Investment, anaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba wa miaka mitano waliouingia.

Magori amesema moja ya maeneo muhimu yaliyopo kwenye mkataba huo ni mchango wa maendeleo ya miundombinu ya klabu, hususan ujenzi wa uwanja wa Simba, ambao unaendelea kupewa kipaumbele na uongozi wa klabu hiyo.

Kwa mujibu wa Magori, mkataba huo unaelekeza kuwa Jayrutty atakuwa akitoa Sh bilioni moja kila mwaka kwa ajili ya kusaidia mradi wa ujenzi wa uwanja, sambamba na fedha nyingine zinazotolewa kwa shughuli za kawaida za udhamini wa jezi.

Amesema utekelezaji wa vipengele vya mkataba huo unaendelea kwa hatua kulingana na muda uliopangwa, akitolea mfano kipengele cha usajili wa mchezaji mmoja kila mwaka ambacho tayari kimeanza kutekelezwa kupitia usajili wa Ino Loemba.

“Utoaji wa basi jipya la Irizar pamoja na mchango wa maendeleo ya uwanja ni sehemu ya mkataba wa miaka mitano. Suala la ujenzi wa uwanja mpya wa Simba limejumuishwa rasmi kwenye mkataba huu ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa klabu,” amesema Magori.

Amefafanua kuwa mdhamini huyo atakuwa akitoa Sh bilioni moja kila mwaka kwa ajili ya mradi wa uwanja, jambo ambalo linaongeza matumaini ya Simba kuwa na uwanja wake ndani ya kipindi cha mkataba huo.

Magori amesisitiza kuwa maamuzi yote yanayohusu ujenzi na usimamizi wa mradi huo yatafanywa chini ya Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, ambayo pia itahakikisha fedha zinazotolewa zinatumika kwa uwazi, ufanisi na kwa mujibu wa malengo yaliyokusudiwa na klabu.

DAR LEOPARDS WALIAMSHA RAGA DAR USA DHIDI YA GERMANY MAPAMBANO KABLA YA KOMBE LA DUNIA