Azam FC

HIMID AWEKA WAZI, SIMBA WASUBIRI, YANGA KWANZA

Vardo June 22, 2026 10:14 am

KIUNGO wa Azam FC, Himid Mao, amesema kikosi hicho hakina muda wa kusherehekea kufuzu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, badala yake kimehamishia nguvu na umakini wake kwenye mchezo muhimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga.

Azam FC ilifanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Yanga katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Hata hivyo, Himid amesema mafanikio hayo sasa yamewekwa pembeni kwa kuwa timu inakabiliwa na mtihani mwingine mgumu dhidi ya wapinzani hao hao katika ligi, mechi itakayochezwa Jumatano, Juni 24, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Kiungo huyo ameeleza kuwa malengo ya Azam kwa sasa ni kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mchezo huo na kuendelea kujiimarisha kwenye mbio za ligi, badala ya kuanza kufikiria fainali inayowasubiri mbele ya Simba SC.

Amesema ushindi walioupata dhidi ya Yanga kwenye nusu fainali unawapa morali kubwa, lakini wanatambua mchezo wa ligi utakuwa tofauti na utahitaji maandalizi makubwa ili kupata matokeo chanya.

Kwa mujibu wa Himid, kikosi chao kinaendelea kufanya maandalizi kwa umakini mkubwa kikilenga kurudia kile walichokifanya katika mchezo uliopita na kuhakikisha wanaondoka na alama tatu muhimu dhidi ya Yanga.

“Ni kweli tunaenda kucheza fainali dhidi ya Simba, lakini hatuwezi kuifikiria mechi hiyo kwa sasa kwa sababu bado ipo mbali. Nguvu na akili zetu zote zipo katika kuhakikisha tunamaliza vizuri mechi zetu za ligi na kusaka ushindi katika mchezo wetu ujao dhidi ya Yanga,” amesema Himid.

RONALDO AIBUA JIPYA MAZOEZINI SIMBA YAJENGA KIKOSI KIPYA, BAADHI YA NYOTA HAWA HATARINI