Yanga SC

YANGA YAMPIGIA MAHESABU BEKI TRA UNITED MSIMU UJAO

Vardo June 26, 2026 5:54 pm

UONGOZI wa Yanga umeanza rasmi harakati za kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu wa 2026/27, huku ukielekeza nguvu katika kuongeza ubora wa safu ya ulinzi kwa kumuweka beki wa kati wa TRA United, Nasri Kombo, kwenye orodha ya vipaumbele vya usajili.

Taarifa zinaeleza kuwa mabosi wa Yanga tayari wameanza mazungumzo ya awali na pande husika kwa lengo la kuona namna ya kukamilisha usajili wa beki huyo, ambaye ameonyesha kiwango bora na utulivu mkubwa katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, benchi la ufundi linaamini Kombo ana sifa zinazoweza kuongeza ushindani katika eneo la ulinzi, hasa wakati timu ikijiandaa kushiriki michuano ya ndani na kimataifa msimu ujao.

Chanzo cha karibu na mchakato huo kimeeleza kuwa mazungumzo yanaendelea katika mazingira mazuri, huku kila upande ukionesha nia ya kufikia makubaliano endapo hakutatokea mabadiliko yoyote katika hatua za mwisho za mazungumzo.

Yanga inalenga kujenga kikosi chenye ushindani mkubwa kitakachokuwa na uwezo wa kutetea mafanikio yake ya ndani pamoja na kufanya vizuri zaidi katika michuano ya kimataifa.

Kombo atakuwa miongoni mwa nyota wapya wanaotarajiwa kujiunga na kikosi hicho, ikiwa ni sehemu ya mpango wa klabu kuimarisha timu kabla ya kuanza kwa msimu mpya.

KINYANGANYIRO CHA UTAWALA NORWAY DHIDI YA UFARANSA, SENEGAL DHIDI YA IRAQ MERIDIANBET YAONYESHA MOYO WA DHAHABU, YAGUSA MAISHA YA FAMILIA BUGURUNI