YANGA YAPEWA DONGO NA SIMBA, WAMESHINDWA KUTUFUNGA, VIPI WAMSAIDIE AZAM
MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema klabu hiyo haina presha na haitishwi na kauli ya Yanga ya kuipa sapoti Azam FC kuelekea fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.
Kauli hiyo imekuja baada ya Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, kueleza kuwa mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, klabu hiyo itaelekeza nguvu zake zote kuisapoti Azam FC katika fainali dhidi ya Simba.
Simba na Azam FC tayari zimefuzu kucheza fainali hiyo inayotarajiwa kufanyika Julai 4, 2026, kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Akizungumza kuhusu kauli hiyo, Ahmed amesema si jambo jipya kwa Yanga kuonyesha sapoti kwa wapinzani wa Simba, akidai kuwa mara nyingi wamekuwa wakifanya hivyo lakini mwisho wa siku Simba imeendelea kupata ushindi.
“Mbona wamekuwa wakiwapa sapoti wapinzani wetu kila tunapocheza nao, lakini mara nyingi wamekuwa wakiangukia pua na sisi tunaondoka na ushindi. Hili si jambo jipya, tofauti ya sasa ni kwamba wameamua kulisema hadharani. Hata yale wanayofanya nyuma ya pazia kwa lengo la kuidhoofisha Simba, juhudi zao zote zimekuwa zikifeli,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa kama Yanga ilikuwa na uwezo wa kuizuia Simba, ingefanya hivyo ilipokutana nayo msimu huu, akisisitiza kuwa imecheza mechi kadhaa dhidi ya Simba bila kupata ushindi.
Ahmed amesema haamini kuwa Yanga inaweza kuipa Azam FC mbinu za kuifunga Simba wakati yenyewe imeshindwa kufanya hivyo.
“Mbinu zilizowashinda wao sidhani kama zinaweza kumsaidia mwingine. Waache waungane na kusaidiana, lakini watamkuta mnyama amesimamisha sharubu kwa ajili ya maangamizi.”
Amesema Simba haioni tatizo kwa Yanga na Azam FC kushirikiana, akisisitiza kuwa kikosi hicho kipo tayari kwa fainali na kina imani ya kuibuka na ushindi.
“Na sisi tunapenda hivyo waungane. Tukimpasua mmoja, maumivu yasambae nchi nzima. Hicho ndicho tunachokisubiri,” alisema Ahmed.