Habari za michezo

MO SALAH HOFU KOMBE LA DUNIA

Vardo June 27, 2026 1:32 pm

Seattle, Marekani: Kocha Mkuu wa Misri, Hossam Hassan, amesema nahodha wa timu hiyo, Mohamed Salah atafanyiwa uchunguzi wa kiafya ili kubaini hali yake baada ya kuomba mwenyewe kutolewa katika mechi dhidi ya Iran, mchezo uliowawezesha Mafarao kufuzu hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026.

Salah ameonekana kutokuwa na furaha dakika ya 57 na akaomba kubadilishwa, jambo lililozua wasiwasi kwa baadhi ya mashabiki waliokuwa wakifuatilia mchezo huo.

Akizungumza baada ya mechi, Hassan amesema bado ni mapema kubaini ukubwa wa tatizo lililompata nyota huyo wa Liverpool, lakini alisisitiza kuwa uamuzi wa kutoka uwanjani ulitokana na ombi la mchezaji mwenyewe.

“Aliomba kutoka uwanjani, na mchezaji anapoomba hivyo maana yake amehisi kuna tatizo. Tutamfanyia vipimo ili kujua hali yake halisi na kumtathmini kwa kina,” amesema Hassan.

Mbali na Salah, kocha huyo amesema beki wa kushoto Ahmed Fatouh naye atafanyiwa uchunguzi baada ya kupata majeraha katika mchezo huo, huku akieleza matumaini kuwa kiungo Hamdi Fathi atakuwa fiti kwa mchezo ujao wa hatua ya 32 bora dhidi ya Australia, baada ya kukosa mchezo dhidi ya Iran kutokana na majeraha.

Licha ya changamoto hizo za majeruhi, Hassan amesema hana wasiwasi na kikosi chake, akisisitiza kuwa ana wachezaji wa kutosha wenye uwezo wa kuziba nafasi ya yeyote atakayekosekana.

“Nina wachezaji wenye uwezo na nina imani nao. Siwezi kuwa na hofu kila mchezaji anapoumia. Kila mmoja ndani ya kikosi hiki anaweza kuchukua jukumu,” amesema.

Kuhusu kufuzu hatua ya mtoano na kuvunja rekodi ya Misri kutofika hatua hiyo katika historia ya Kombe la Dunia, kocha huyo alisema mafanikio hayo si ya Misri pekee bali ni fahari kwa Afrika na ulimwengu wa Kiarabu.

“Haya ni mafanikio makubwa kwa Misri, kwa Afrika na kwa ulimwengu wa Kiarabu, lakini kazi bado haijaisha. Tutajiandaa vizuri na kupambana kwa kila hali katika hatua inayofuata,” ameongeza.

Misri ilifuzu hatua ya 32 bora baada ya kumaliza nafasi ya pili katika Kundi G ikiwa na pointi tano, sawa na Ubelgiji, lakini ikapishana kwa tofauti ya mabao.

Misri sasa itacheza dhidi ya Australia katika hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026, mchezo unaotarajiwa kupigwa Ijumaa, Julai 3, 2026, kuanzia saa 4:00 usiku (saa za Marekani) katika Uwanja wa Dallas, Arlington, Texas, Marekani.

MKATABA WA M’MOMBWA, ZABBAR UTATA