Neymar Atangaza Kustaafu Timu Ya Taifa Ya Brazil
LOS ANGELES, MAREKANI: NYOTA wa Brazil, Neymar, ametangaza kustaafu soka la kimataifa baada ya Brazil kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2026 kufuatia kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Norway.
Neymar alicheza mechi mbili pekee kwenye Kombe la Dunia la mwaka huu na kufunga bao la penalti katika dakika za mwisho za mechi yake ya mwisho akiwa na jezi ya Brazil, lakini bao hilo halikutosha kuizuia timu hiyo kupata moja ya matokeo mabaya zaidi katika historia yake ya Kombe la Dunia, ikiondolewa mapema zaidi tangu mwaka 196Baada ya filimbi ya mwisho, Neymar alionekana akitokwa na machozi, ishara iliyozidisha taarifa zilizokuwa zikienea kwa muda kwamba angehitimisha safari yake ya kimataifa baada ya mashindano hayo.
Kocha Carlo Ancelotti alikuwa amemrejesha Neymar kikosini baada ya kukaa nje ya timu ya taifa kwa takribani miaka mitatu, akimpa nafasi ya mwisho ya kutimiza ndoto ya kunyanyua Kombe la Dunia. Hata hivyo, ndoto hiyo ilifutwa na straika wa Norway, Erling Haaland, aliyefunga mabao mawili ya ushindi.
Licha ya kipigo hicho, Ancelotti amesema hatajiuzulu na badala yake ataendelea kuijenga upya Brazil.
“Kipigo hiki kinauma, lakini bado nina hamasa ya kuendelea na kazi. Tunahitaji damu changa zaidi katikati ya uwanja na wachezaji wa kiwango cha juu watakaobeba timu siku zijazo,” alisema Ancelotti.
Akizungumza muda mchache baada ya kutangaza uamuzi huo, Neymar alisema kuwa amejaribu mara nyingi kuhakikisha kuwa anafanya vizuri kwenye michuano hiyo, lakini jambo hilo limeshindikana na hana haja ya kulazimisha zaidi.
“Nimejaribu sana, nilianzia hapa Met Life, na nimemalizia hapa. Sasa ni mwisho.”