Haaland Alivyoikatili Brazil Kombe La Dunia
Brazil imeaga fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kufungwa mabao 2-1 na Norway katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa kwenye Uwanja wa New York/New Jersey, Marekani.
Haaland alifunga bao la kwanza kwa kichwa dakika ya 80, baada ya kumzidi ubabe beki Gabriel Magalhães katika pambano lao la ana kwa ana lililodumu kwa muda wote wa mechi.
Mshambuliaji huyo wa Manchester City alionyesha kwa mara nyingine kuwa hahitaji kugusa mpira mara nyingi ili kuamua matokeo ya mchezo. Bao lake la sita katika Kombe la Dunia lilitokana na mguso wake wa 21 pekee, likiiweka Brazil kwenye hali ya kukata tamaa ambayo hata kocha Carlo Ancelotti hakuweza kuibadili.
Mbali na Haaland, kipa Orjan Nyland alikuwa nguzo muhimu ya ushindi wa Norway. Aliokoa penalti ya mapema ya Bruno Guimarães dakika ya 14, akamzuia Vinícius Júnior na Rayan wasifunge, kabla ya kuzuia kwa ustadi mpira uliokuwa ukielekea wavuni kutoka kwa mwenzake Kristoffer Ajer ambao ungeweza kuwa bao la kujifunga.
Brazil ilifanikiwa kupata bao moja kupitia Neymar Jr kwa penalti dakika ya 90+10, lakini halikutosha kuizuia Norway kuandika ushindi wa kihistoria.