Jux Na Priscilla Ojo Waweka Rekodi Ya Kihistoria Instagram Tanzania
Zimesalia siku chache tu kutimia mwaka mmoja tangu staa wa Bongofleva, Jux na mkewe Priscilla Ojo, wateke hewa kwenye mtandao wa Instagram. Chapisho lao la pamoja lililowekwa Julai 2025 hadi sasa linashikilia rekodi ya kuwa na mwingiliano (engagement) mkubwa zaidi kuliko staa yeyote nchini Tanzania.
Priscilla, ambaye ni binti wa mwigizaji mashuhuri wa Nollywood, Iyabo Ojo, pamoja na Jux, wanatajwa kuwa miongoni mwa mastaa wenye ushawishi mkubwa zaidi mtandaoni. Wawili hao walianza kuweka wazi uhusiano wao mnamo Julai 2024, miezi michache baada ya Jux kuachana na aliyekuwa mpenzi wake, Karen Bujulu.
Posti Ilivyovunja Rekodi ya Likes Milioni 1.1 Mnamo Julai 24, 2025, wawili hao walichapisha picha za pamoja zilizosindikizwa na maneno, “Mom & Dad. Blessed, grateful, thankful,” wakithibitisha kuwa walikuwa wanatarajia mtoto wao wa kwanza baada ya tetesi za muda mrefu.
Hadi sasa, chapisho hilo limevunja rekodi nchini Tanzania kwa kufikisha:
-
Likes: Milioni 1.1
-
Maoni (Comments): 91,500
-
Kusambazwa (Shares): 110,000
Kwa muktadha wa kidunia, rekodi ya chapisho lenye likes nyingi zaidi bado inashikiliwa na nguli wa soka Lionel Messi, aliyepata likes milioni 74.5 baada ya kuinua Kombe la Dunia mnamo Desemba 2022.
Zawadi ya Wimbo na Kuzaliwa kwa Mtoto Rakeem Siku hiyohiyo walipotangaza ujauzito, Jux aliachia wimbo maalum uitwao “Thank You” (2025) uliotayarishwa na S2kizzy na kuongozwa na Director Kenny, kama shukrani kwa mkewe. Hiyo ilikuwa video ya nne kwa Priscilla kutokea kama vixen wa Jux, baada ya nyimbo kama Ololufe Mi (2024), Si Mimi (2025), na God Design (2025) kutoka kwenye EP yake ya A Day To Remember.
Mwishoni mwa Agosti 2025, wawili hao walibarikiwa kupata mtoto wa kiume nchini Canada waliyempa jina la Rakeem. Jux alieleza kuwa walichagua Canada ili kumpa mtoto wao fursa ya kuchagua uraia anaoutaka atakapofikisha miaka 18.
Ukuaji wa Nguvu ya Ushawishi (Brand Influence) Tangu aingie kwenye mahusiano na Jux, wafuasi wa Priscilla Instagram wameongezeka kutoka milioni 2.8 hadi kufikia milioni 4.7 (ongezeko la wafuasi milioni 1.9). Hatua hii imemwongezea dili kubwa za ubalozi wa chapa mbalimbali kama vile ChiJ14Exchange, Viskit, na Hegai & Esther.
Akizungumza kwenye podcast ya Chude Jideonwo, Priscilla alifichua kuwa walikutana kwa mara ya kwanza nchini Rwanda ambapo Jux alivutiwa naye na kuomba namba yake. Aliongeza kuwa mwanzoni walipanga kuwa na watoto 16, lakini baada ya kupata wa kwanza, mipango hiyo imebadilika.
Wawili hao walifunga ndoa rasmi Februari 7, 2025, sherehe zilizofuatiwa na matukio ya kifahari nchini Nigeria na kilele chake kuwa Mei 28, 2025, katika ukumbi wa The Superdome. Licha ya uvumi mtandaoni kuwa Jux alikopa Shilingi Bilioni 1 kufanikisha harusi hiyo, msanii huyo alikanusha vikali madai hayo.