Ahmed Ally Simba SC
Simba SC

Ahmed Ally Awatuliza Wanasimba Sakata la Selema Mwalimu

Vardo August 11, 2026 8:08 pm

Sakata la aliyekuwa mshambuliaji wa Simba SC, Selema Mwalimu, kutambulishwa na klabu nyingine limechukua sura mpya na kuibua taharuki kubwa miongoni mwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi. Hata hivyo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amewataka Wanasimba kutulia na kuelekeza akili zao zote kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC.

Sintofahamu hiyo iliongezeka baada ya mchezaji huyo—ambaye awali alitambulishwa rasmi katika kilele cha Simba Day—kuonekana tena akitambulishwa na klabu nyingine, jambo lililoacha maswali mengi bila majibu kwa mashabiki.

Akizungumza kuhusu hali hiyo, Ahmed Ally aliwapa pole mashabiki na kuwataka kutoshtushwa na kinachoendelea, akisisitiza kuwa kipaumbele cha klabu kwa sasa ni mchezo wa ufunguzi wa msimu.

“Wengi tumeingia kwenye taharuki baada ya kuona aliyekuwa mshambuliaji wetu akitambulishwa klabu nyingine. Taharuki kubwa zaidi inatokana na sisi kumtambulisha mchezaji husika kwenye siku wetu tukufu ya Simba Day,” alisema Ahmed Ally.

“Kwanza niwape pole Wanasimba kwa taharuki hii. Sipo hapa kujielezea nini kimetokea, kitu muhimu zaidi kwa sasa ni kuweka nguvu kwenye mchezo wetu wa kesho wa Ngao ya Jamii.”

Lengo Kuu: Kurejesha Taji la Ngao ya Jamii Msimbazi

Simba SC inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na kiu kubwa ya ushindi baada ya kukosa taji la Ngao ya Jamii kwa misimu miwili mfululizo. Ahmed Ally amebainisha kuwa huu ndio wakati sahihi wa Simba kuanza msimu mpya kwa kutwaa ubingwa huo.

Ni kitu gani tunachohitaji zaidi ya ushindi? Kwa misimu miwili tumeikosa Ngao ya Jamii. Huu ndio wakati sahihi wa kuchukua taji hili, Insha Allah. Akili yetu, fikra zetu, mawazo yetu na nguvu zetu tuzielekeze Amaan Stadium. Safari hii tunatakiwa kuufungua msimu kwa ubingwa,” aliongeza Ahmed.

Akimalizia amewasihi mashabiki kuendelea kuipa timu ushirikiano wa dhati bila kuruhusu mambo ya nje ya uwanja kuwavuruga kuelekea pambano hilo la ushindani mkubwa huko Amaan Stadium, Zanzibar.

“Tumerithishwa kuipenda Simba yetu, hivyo tuendelee kuipigania kesho tupate furaha ya wote. Let’s go Wanasimba. Punje ya mchele ikidondoka, wali utaliwa tu.”

HISTORIA: Malawi Yaingia Nusu Fainali WAFCON na Kufuzu Kombe la Dunia 2027! Yanga SC Yaongeza ‘Risasi’ Mbele: Mwalimu Aongeza Ushindani Msimu Wa 2026/27