Diamond na Trey Songz
Burudani

Diamond na Trey Songz Wafanya Maajabu Jukwaani Dar, Waimba ‘Big Money’

Vardo August 15, 2026 11:23 am

Staa wa Bongofleva, Diamond Platnumz, amewashangaza na kuwasisimua mashabiki kwenye Tamasha la Imbeju Sauti Moja lililofanyika Viwanja vya Posta, Dar es Salaam, baada ya kutokea jukwaani kwa shtukiza wakati msanii wa R&B kutoka Marekani, Trey Songz, akiendelea kutoa burudani.

Trey Songz alikuwa akifanya onyesho lake la kwanza kabisa nchini Tanzania, akiwakutanisha mashabiki na muziki wake wa R&B katika usiku uliojaa hisia na burudani ya kiwango cha juu. Hata hivyo, msisimko uliorogeshwa zaidi Diamond alipopanda jukwaani na kusababisha umati wote kulipuka kwa shangwe huku sauti za “Simba! Simba!” zikitawala eneo lote la viwanja hivyo.

Kupanda kwa Diamond jukwaani hakukuishia tu kwenye kusalimiana; wawili hao walitumia fursa hiyo kuwazawadia mashabiki burudani ya kipekee kwa kutumbuiza pamoja kwa mara ya kwanza wimbo wao mpya unaoitwa ‘Big Money’, ambao bado haujatolewa rasmi.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Diamond na Trey Songz kuonekana wakitumbuiza pamoja nchini Tanzania, jambo lililoongeza uzito mkubwa kwani ushirikiano (collabo) wao umekuwa ukingojewa kwa hamu kubwa na mashabiki wa muziki.

Diamond alionyesha uzoefu na kujiamini kwa hali ya juu jukwaani, akimpa sapoti Trey Songz na kuungana naye kwenye sehemu mbalimbali za wimbo huo. Uwezo wake wa kuichangamsha hadhira ulionekana wazi, kwani kila aliposhika maiki, mashabiki walipaza sauti kumshangilia.

Kwa upande wake, Trey Songz alionekana kufurahia sana uwepo wa Diamond, akishuhudia mwenyewe namna staa huyo wa Bongo Flava anavyoweza kubadilisha upepo wa tamasha ndani ya sekunde chache. Wakati wa onyesho hilo, Trey alimwachia Diamond nafasi ya kuongoza jukwaa huku yeye akiimba sauti za nyuma (backing vocals).

Tukio hili limeongeza hamu kubwa miongoni mwa mashabiki wanaosubiri kwa hamu kutoka rasmi kwa wimbo wa ‘Big Money’. Performance hii kwenye Tamasha la Imbeju Sauti Moja inabaki kuwa miongoni mwa matukio ya kihistoria katika usiku ambao Trey Songz aliandika kumbukumbu mpya nchini Tanzania.

Namungo vs Yanga Leo: Mtihani Mzito Ruangwa | Ligi Kuu Tanzania Bara Somo la Trey Songz kwa Wasanii wa Tanzania: Tamasha la Imbeju Sauti Moja