Usajili wa Yanga Gelson Dala: Utambulisho wa X Factor Mpya KMC Complex
SAA na Dakika zikisogea, ndivyo hamu ya mashabiki wa Yanga inavyopanda, huku klabu hiyo ikikaribia kukamilisha usajili wa ‘X Factor’ wake mpya, Gelson Dala, kiungo mshambuliaji wa Al-Wakrah ya Qatar na raia wa Angola.
Jioni ya leo, mabingwa hao wa Tanzania wanaendelea na hatua za mwisho za kukamilisha dili hilo na kumtambulisha nyota huyo mwenye uzoefu mkubwa wa soka la ushindani.
Taarifa zinaeleza kuwa Yanga tayari imefanya mazungumzo ya moja kwa moja na Dala, huku pande hizo zikielekea kukamilisha makubaliano kabla ya dirisha la usajili kufungwa.
Dala anatajwa kuwa mchezaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja katika safu ya ushambuliaji, akimudu kucheza kama kiungo mshambuliaji namba 10 na pia mshambuliaji wa kati namba tisa.
Uwezo huo unatarajiwa kumpa Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, chaguo pana zaidi katika kupanga kikosi chake, hasa kutokana na msimu mpya kuwa na ushindani mkubwa katika mashindano ya ndani na kimataifa.
Yanga imekuwa ikifanya usajili wa nguvu kuelekea msimu mpya ikiwa na lengo la kujenga kikosi imara kitakachoweza kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, sambamba na kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
Kwa sasa, Dala ndiye anayetajwa kuwa usajili wa mwisho wa Yanga katika dirisha hili, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kubwa muda wa kutambulishwa kwake katika KMC Complex.
Dirisha la usajili likielekea kufungwa saa 6:00 usiku, macho ya mashabiki wa Yanga yameelekezwa kwenye hatua za mwisho za dili hilo, ambalo likikamilika linaweza kuwa miongoni mwa usajili utakaozungumziwa zaidi katika dirisha hili.