Mngqithi Afichua Mtego wa Peter Shalulile Yanga SC
KOCHA Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amefunguka na kuweka wazi kuwa hana wasiwasi wowote na kiwango cha mshambuliaji wake, Peter Shalulile, huku akisisitiza kuwa uwepo wa nyota huyo utazidi kuwa tishio kubwa kwa mabeki wa timu pinzani msimu huu.
Mngqithi ameeza kuwa Shalulile ni aina ya mshambuliaji wa kipekee anayejua kuweka presha ya mara kwa mara kwa mabeki kupitia nguvu, kasi na harakati zake uwanjani. Hali hiyo imekuwa ikiwalazimisha wapinzani kufanya makosa makubwa ndani ya eneo lao la hatari.
Kocha huyo aliongeza kuwa hata katika michezo ambayo Shalulile anaonekana kutokutakata kikamilifu, uwepo wake pekee uwanjani unatosha kuleta taharuki na hofu kubwa kwa safu ya ulinzi ya mpinzani, jambo linalowafanya wakati mwingine wajikute wakimzawadia nafasi za wazi za kufunga.
“Siwezi kuwa na shaka na Shalulile. Ni mchezaji ambaye muda wowote anaweza kusababisha madhara makubwa kwa mabeki. Wakati mwingine mabeki wanakuwa kwenye hofu kubwa kiasi kwamba wanajikuta wakimzawadia mabao,” amesema Mngqithi.
Kadiri Shalulile atakavyozidi kuzoea mfumo na muunganiko wa wachezaji wenzake, Mngqithi anaamini uwezo wake wa kupasua safu za ulinzi utaongezeka mara dufu, hasa pale Yanga inapokabiliana na timu zinazocheza mpira wa kujilinda.
Pia amesisitiza kuwa kikosi cha Yanga bado kipo kwenye mchakato wa kujenga muunganiko thabiti zaidi, hivyo mashabiki watarajie kuona kiwango cha timu na wachezaji mmoja mmoja kikizidi kuimarika kadiri msimu unavyosogea. Kauli hii ya kocha inaonyesha imani kubwa aliyonayo kwa Shalulile kuwa silaha kuu ya kutetea mafanikio ya klabu msimu huu.