Sunderland Yaingia Mkataba wa Sh68 Bilioni Kumsajili Dayann Methalie wa Toulouse
SUNDERLAND, UINGEREZA – Klabu ya Sunderland imefikia makubaliano ya kumsajili beki wa kushoto wa Toulouse, Dayann Methalie, kwa ada ya jumla ya pauni milioni 25.6 (takribani Shilingi bilioni 68 za Kitanzania).
Miamba hiyo miwili imekubaliana ada ya msingi ya pauni milioni 23.9, huku pauni milioni 1.7 zikiwa ni bonasi zitakazolipwa kulingana na utendaji wa mchezaji huyo uwanjani pamoja na masharti mengine ya mkataba.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 20 na raia wa Ufaransa anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya muda wowote kuanzia sasa kabla ya kukamilisha taratibu zote za kujiunga na Sunderland.
Msimu uliopita akiwa na Toulouse, Methalie alionyesha kiwango cha juu baada ya kucheza mechi 28 za Ligue 1 na kufanikiwa kufunga mabao mawili katika michezo yake tatu ya mwisho. Mchango wake uliisaidia Toulouse kumaliza katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi kuu nchini Ufaransa, kiwango kilichowashawishi mabosi wa Sunderland kumwaga fedha hizo ili kunasa saini yake katika dirisha hili la usajili.