Kiungo wa Tanzania Alphonce Mabula Kutua JS Kabylie ya Algeria Kwa Mkataba Mnene!
KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Alphonce Mabula, yuko mbioni kuandika ukurasa mpya na wa kihistoria katika maisha yake ya soka baada ya kuondoka nchini kuelekea Algeria kukamilisha uhamisho wake wa kujiunga na miamba ya soka ya nchi hiyo, JS Kabylie.
Mabula tayari ameshaondoka Tanzania na kuwasili Algeria, ambapo anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kumalizia hatua za mwisho za kusaini mkataba na miamba hiyo yenye heshima kubwa barani Afrika.
Uhamisho huu unatajwa kuhusisha kitita kikubwa cha fedha, jambo linaloashiria thamani kubwa aliyonayo mchezaji huyo. Hii ni hatua kubwa na muhimu katika safari yake ya soka, kwani anenda kuanza maisha mapya kwenye ligi yenye ushindani na mbinu za hali ya juu.
JS Kabylie ni moja ya klabu kongwe, tajiri na zenye mafanikio makubwa zaidi nchini Algeria na barani Afrika kwa ujumla. Kutua kwa Mabula klabuni hapo kunampa jukwaa zuri la kuonyesha na kupima uwezo wake katika kiwango cha juu cha soka la kimataifa.
Kwa sasa, mashabiki wa soka nchini Tanzania na Algeria wanasubiri kwa hamu kutambulishwa kwake rasmi mara tu taratibu zote zitakapokamilika. Safari hii ya Mabula inaendelea kufungua milango na kuongeza idadi ya wachezaji wa Kitanzania wanaosaka mafanikio katika vilabu vikubwa vya soka barani Afrika.