Ibrahim Doumbia Afunguka Ukimya Wa Mabao Simba SC, Atuma Ujumbe Mzito!
MSHAMBULIAJI mpya wa Simba SC, Ibrahim Doumbia, amewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo kuhusu ukimya wake wa kutopachika mabao katika michezo ya awali ya msimu huu, akisisitiza kuwa muda wake wa kufungua akaunti ya mabao utafika hivi karibuni.
Doumbia, ambaye anaendelea kupigania namba katika kikosi cha kwanza cha Simba, ameeleza kuwa kila mshambuliaji anatamani kufunga kila anapopata nafasi, lakini kwake hali hiyo haimwekei presha yoyote kwa kuwa ligi bado ni mbichi.
Amebainisha kuwa kinachompa amani kwa sasa ni kuendelea kufanya kazi kwa bidii mazoezini, kufuata maelekezo ya walimu, na kutumia vizuri kila fursa anayopata ili kujenga kujiamini kadiri msimu unavyozidi kuchanganya.
“Ni mara ya kwanza kabisa kwangu kupitia kipindi cha aina hii, kwa sababu hii ni ligi ambayo ndiyo kwanza imeanza. Kwa hiyo ni jambo la kawaida, hasa unapokuwa unapata nafasi yako ya kwanza,” amesema Doumbia.
Mshambuliaji huyo ameongeza kuwa mashabiki wanapaswa kuvuta subira kwani bado kuna michezo mingi mbele, na kutofunga kwa sasa haimaanishi kwamba hana uwezo wa kuibeba safu ya ushambuliaji ya Wekundu wa Msimbazi.
Simba inatarajia mchango mkubwa kutoka kwa Doumbia msimu huu katika mashindano ya ndani (Ligi Kuu na Kombe la FA) pamoja na mechi za kimataifa, huku benchi la ufundi likiamini uwezo wake wa kuongeza nguvu na ukali kwenye eneo la mwisho la ushambuliaji.