Nahodha Kenya U-20: Tumeja CECAFA Kutwaa Taji na Kukata Tiketi ya AFCON
NAHODHA wa timu ya taifa ya Kenya ya vijana chini ya umri wa miaka 20 (Kenya U-20), Charles Junior, ameeleza kuwa kushiriki katika mashindano ya CECAFA U-20 ni hatua kubwa na fursa ya dhahabu kwa wachezaji kujitangaza na kuonyesha uwezo wao kimataifa.
Akizungumza kuhusu michuano hiyo, Junior amebainisha kuwa mbali na kusaka ubingwa, mashindano hayo yanawapa vijana jukwaa muhimu la kujifunza, kujijenga pamoja na kupata uzoefu wa kukutana na wapinzani wa ngazi mbalimbali barani Afrika.
Hata hivyo, kiungo huyo anayechezea klabu ya Sofapaka FC nchini Kenya, amesisitiza kuwa kikao chao hakijaja kwenye mashindano hayo kama washiriki tu, bali wana kiu ya kuandika historia.
“Lengo letu kubwa ni kubeba taji. Tunataka kufanya vizuri na kuhakikisha tunafuzu kwenda kucheza AFCON,” alisema Junior.
Nahodha huyo aliongeza kuwa safari ya kuelekea Fainali za AFCON U-20 zitakazofanyika Ghana mwaka 2027 haitakuwa nyepesi kutokana na ushindani mkali uliopo. Ili kufikia malengo hayo, ametoa wito kwa wachezaji wenzake kupambana kwa nidhamu, kufuata maelekezo ya benchi la ufundi na kucheza kwa ushirikiano wa hali ya juu.