Kazi Imeanza! Ibenge Afichua Mpango Mzito Kikosi cha Azam FC Wakati wa Kalenda ya FIFA
Kocha Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, ametumia mapumziko ya kalenda ya FIFA kuanza mchakato mzito wa kukinoa na kukijenga upya kikosi chake, huku akiweka wazi mpango wa kucheza mechi mbili za kirafiki kabla ya kuwakabili Coastal Union.
Licha ya Azam FC kuwakosa wachezaji 12 waliitwa kwenye timu zao za taifa za wakubwa, vijana chini ya miaka 20 (U-20) na miaka 23 (U-23), Ibenge amesema pengo hilo halitasimamisha mipango ya timu, bali ni fursa ya kuongeza ushindani kwa wachezaji waliosalia.
“Tumekuwa na wachezaji wengi walioenda kutekeleza majukumu ya timu za taifa, wakiwemo wa vikosi vya vijana U-20 na U-23. Kwa ujumla ni wachezaji 12 tunaowakosa,” alieleza Ibenge.
Kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa alifafanua kuwa wachezaji waliobakia wanaendelea na programu maalum ya kuimarisha utimamu wa mwili. Mazoezi yalianza asubuhi kwa kujenga misuli gym kabla ya kuhamia uwanjani kwa ajili ya mbinu za ufundi (tactics). Aidha, ili kufidia idadi ya wachezaji mazoezini, benchi la ufundi limepanda na vijana kadhaa kutoka kwenye akademi ya klabu hiyo.
“Kwa wale waliosalia, lazima tuhakikishe tunapandisha ubora wao. Sio kitu kigumu kwa sababu tuna vijana wengine kwenye akademi yetu ambao tunaweza kuwatumia kukamilisha kikosi chetu cha mazoezi,” aliongeza.
Ibenge alihitimisha kwa kufichua kuwa wana mpango thabiti wa kucheza mechi mbili za kirafiki ili kupima ubora wa kikosi hicho kabla ya mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union, hatua inayowapa uhakika mashabiki kuwa timu yao inazidi kuimarika.