Sintofahamu Uwanja wa Simba SC Ligi ya Mabingwa Afrika Yashika Kasi
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amefichua sintofahamu nzito inayoendelea kuhusu uwanja utakaotumika kwa mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya 15 de Agosto ya Equatorial Guinea, huku Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likiwa limetoa maelekezo ya awali.
Akizungumza kuhusu kadhia hiyo, Ahmed amesema mkanganyiko huo umeanza baada ya kujitokeza kwa changamoto ya upatikanaji wa uwanja kwa wapinzani wao. Hali hiyo iliilazimu Simba kufanya mawasiliano ya haraka na klabu hiyo mara tu baada ya kufahamu kuwa watakutana katika hatua hiyo ya mashindano ili kupata muafaka wa eneo la mchezo wa kwanza.
Hata hivyo, juhudi za awali za Simba hazikuzaa matunda kwa wakati, jambo lililoifanya klabu hiyo kuwasilisha suala hilo rasmi kwa CAF, ambayo nayo iliingilia kati na kuwasiliana na 15 de Agosto kupata ufafanuzi wa mahali ambapo pambano hilo lingepigwa.
Kutokana na ukimya na kuchelewa kupatikana kwa majibu, Ahmed alifafanua kuwa CAF ilitoa maelekezo ya michezo yote miwili kuchezwa jijini Dar es Salaam. Pamoja na maelekezo hayo, mambo hayajaisha bado kwani 15 de Agosto wameanzisha mawasiliano mapya na shirikisho hilo wakishinikiza mchezo wa mkondo wa kwanza uamie nchini Congo.
“Kwa sasa wenzetu wa 15 de Agosto wanaendelea kufanya mawasiliano na CAF ili mechi ichezwe Congo. Sisi tumepokea maelekezo kwamba mechi itachezwa Dar es Salaam, lakini yote kwa yote tunasubiri uamuzi wa mwisho wa CAF ili tujue watatuelekeza nini na tuweze kuwapa taarifa mashabiki wetu,” amesema Ahmed.
Wakati mambo yakiwa bado njia panda, Simba imewataka mashabiki na wanachama wake kuwa watulivu na kuendelea kufuatilia taarifa rasmi zitakazotolewa na klabu hiyo mara tu baada ya CAF kufikia uamuzi wa mwisho kuhusu pamabano hilo la kimataifa.