Simba SC Yamwaga Tabasamu CAF: Mechi Zote za Raundi ya Pili Zichezwa Dar!
SIMBA SC imepata nafuu kubwa ya kimkakati baada ya kupata nafasi ya kucheza mechi zote mbili za raundi ya pili ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya 15 de Agosto ya Equatorial Guinea kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Uamuzi huu unaiwezesha timu hiyo kupunguza gharama za usafiri na kujiandaa katika mazingira rafiki na yanayofahamika.
FAIDA YA KUPIGA MECHI NYUMBANI
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kucheza mechi hizo zote jijini Dar es Salaam kutakuwa na manufaa makubwa kwa timu hiyo, ikiwemo kupunguza gharama za safari, kuondoa usumbufu wa kusafiri nje ya nchi, na kuwatumia mashabiki wao kikamilifu.
Ahmed amesema hali hiyo inairuhusu Simba kuelekeza nguvu zake zote katika maandalizi ya kiufundi badala ya kupoteza muda mwingi kwenye safari ndefu.
“Faida ni kubwa sana kwa sababu hatupati tena muda wa kusafiri. Kwa kukaa hapa hapa, maana yake tuko nyumbani, tunatumia viwanja vyetu na kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Uhuru. Ni rahisi sana,” amesema Ahmed.
SINTOFAHAMU YA TAREHE YATUA MWANGA
Akizungumzia maandalizi ya kikosi hicho, Ahmed ameeleza kuwa Simba iliamua kurejea haraka mazoezini kutokana na kutokufahamika kwa tarehe rasmi za michezo hiyo hapo awali, hali iliyomlazimu kocha kuendelea na programu bila kupoteza muda. Awali, kulikuwa na uwezekano wa mechi kuchezwa Oktoba 16, 17, 18, au 20.
Hata hivyo, mambo yako sawa sasa! Mechi ya mkondo wa kwanza itapigwa Oktoba 20, na marudiano ni Oktoba 25, zote zikianza saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Uhuru.
Kwa upande wa Simba, hii ni fursa ya dhahabu ya kutumia vizuri uwanja wa nyumbani kuhakikisha wanatinga hatua inayofuata kwa kishindo.