Prince Dube Afunguka: Siwezi Kuisaliti Yanga Kwenda Simba SC
Mshambuliaji hatari wa zamani wa Yanga SC, Prince Dube, amevunja ukimya na kukanusha vikali taarifa zilizokuwa zikimhusisha na mpango wa kujiunga na watani wao wa jadi, Simba SC, akisisitiza kuwa bado anayo nafasi kubwa ya mapenzi na klabu hiyo ya Jangwani.
Jina la Dube lilikuwa limetajwa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii likihusishwa na dirisha dogo la usajili ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi, huku kukiwa na madai kuwa anatafutwa kwenda kuziba pengo la Ibrahim Doumbia.
Hata hivyo, akizungumzia uvumi huo, Dube ameweka wazi kuwa hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika kati yake na uongozi wa Simba, akifafanua kuwa kuondoka kwake Yanga hapo awali hakukutokana na kuichoka klabu hiyo, bali ilikuwa ni kutokana na masuala ya mkataba na azma yake ya kurejea nyumbani.
“Niliomba uongozi uniruhusu nisiongeze mkataba ili nirudi nyumbani kucheza soka la hapa. Ikitokea ningetamani kuendelea kubaki, basi mpaka sasa ningekuwa bado nipo Yanga,” alisema Dube.
Mchezaji huyo ameongeza kuwa uhusiano wake na uongozi pamoja na mashabiki wa Yanga umemfanya aione timu hiyo kuwa sehemu maalum ya maisha yake ya soka, akisisitiza kuwa endapo atarejea kucheza nchini Tanzania, Yanga itakuwa chaguo lake la kwanza na la pekee.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kushawishiwa kuhamia upande wa pili wa pili (Simba), Dube alijibu kwa msisitizo mkubwa:
“Kurudi Tanzania halafu kwenda kucheza kwa mahasimu wa Yanga ni usaliti mkubwa sana. Siwezi, siwezi kabisa.”
Kauli hii inazima rasmi minong’ono yote ya usajili iliyokuwa ikienea mitaani na kuwapa utulivu mashabiki wa Yanga ambao bado wanamkumbuka mshambuliaji huyo mahiri.