Diamond Platnumz Aweka Historia Kubwa Afrika, Atwaa Tuzo ya ‘Top African Celebrity 2026’!
SUPASTAA wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, ameendelea kuimarisha na kutawala ramani ya burudani barani Afrika baada ya kutajwa rasmi kuwa mshindi wa tuzo ya Top African Celebrity of the Year 2026.
Mafanikio haya yanazidi kuimarisha ushawishi wake mkubwa kimataifa, huku rekodi zikionyesha kuwa yeye ndiye msanii wa kwanza kuchukua tuzo hiyo inayotolewa na Africa Golden Awards 2026, ambayo hufanya kazi na mastaawakubwa duniani akiwemo Davido, Ne-Yo, Omarion, na Alicia Keys.
Mataji na Ushirikiano wa Kimataifa
Diamond, ambaye pia ni kiongozi wa lebo ya WCB Wasafi, amekuwa akitumia muziki wake kujitanua nje ya mipaka ya Tanzania kwa miaka mingi. Kupitia albamu zake nne na ushirikiano na wasanii kama Koffi Olomide, Rick Ross, Morgan Heritage, Tiwa Savage, na Davido, amefanikiwa kuendelea kubeba bendera ya Bongo Fleva kwenye masoko mapana ya kimataifa.
‘Joy’ Yampa Ushindi Mwingine Mkubwa
Mafanikio ya staa huyu hayakuishia hapo. Kupitia wimbo wake mtamu wa “Joy” aliomshirikisha Juma Jux, wawili hao walijinyakulia tuzo ya Best Collaboration kwenye tuzo za African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2026 zilizofanyika Dallas, Texas, Marekani. Wimbo huo umeendelea kufanya vizuri na kutazamwa na zaidi ya watu milioni 19 kwenye mtandao wa YouTube ndani ya miezi sita tangu utoke, jambo linaloonyesha nguvu ya ushirikiano wa wasanii wa nyumbani.
Zaidi ya Miaka 16 ya Mafanikio
Akiwa kwenye tasnia ya muziki kwa zaidi ya miaka 16 tangu kuachia wimbo wake wa kwanza Kamwambie mwaka 2010, Diamond amethibitisha kuwa mafanikio yake ya kimuziki na uwekezaji wake katika biashara za burudani ni mfano wa kuigwa. Mchanganyiko huu wa uwekezaji na sanaa unaendelea kumfanya kuwa msanii anayefuatiliwa kwa karibu zaidi na mamilioni ya mashabiki Afrika na duniani kote.