Kyle Walker Avunja Ukimya: Aweka Wazi Mpango wa Kufuta Tattoo ya Mataji Manne ya Man City!
Beki wa zamani wa Manchester City, Kyle Walker, amewashangaza wengi baada ya kukiri kwamba atalazimika kufuta tattoo yake maarufu inayoadhimisha mafanikio ya kihistoria ya kutwaa mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu England, iwapo klabu hiyo itanyang’anywa mafanikio hayo kutokana na sakata la ukiukaji wa kanuni za kifedha.
Walker, mwenye umri wa miaka 36 na ambaye kwa sasa anakipiga klabu ya Burnley katika michuano ya Championship, anakuwa mchezaji wa kwanza wa zamani wa Man City kuzungumza waziwazi kuhusu tuhuma hizo zinazoikabili klabu hiyo yenye makao yake Etihad.
Akizungumza kupitia kipindi cha talkSPORT Drive!, beki huyo mahiri alieleza kusikitishwa na hali hiyo lakini akasisitiza kuwa hawezi kufuta mchango mkubwa walioutoa uwanjani kama wachezaji.
“Huenda ikabidi nifanye hivyo (kufuta tattoo), lakini tusifiche ukweli kwamba klabu imepatikana na hatia na inaendelea na rufaa. Kama mchezaji, ninachoweza kusema ni kwamba tulichofanya ni kwenda uwanjani na kucheza soka letu bora. Nitatetea wachezaji wenzangu kwa maisha yangu yote,” alisema Walker.
Manchester City inakabiliwa na tishio kubwa la kuchukuliwa hatua kali za kisheria na kinidhamu—pamoja na uwezekano wa kufukuzwa kwenye Ligi Kuu England—kutokana na tuhuma zaidi ya 100 zinazohusisha kuongeza mapato ya klabu kwa zaidi ya pauni milioni 900 kupitia mikataba tata ya udhamini kati ya mwaka 2009 na 2018.
Licha ya hali hiyo kuwa ngumu kwa mashabiki, Walker anatumaini kuwa juhudi zao za jasho uwanjani hazitafutika kwenye vitabu vya historia.