Muembe Makumbi City
Michezo Bongo

Muembe Makumbi City Yatangaza Lengo Zito Ligi Kuu Zanzibar

Vardo October 23, 2026 8:56 pm

Beki mahiri wa timu ya Muembe Makumbi City, Jumbe Bakari Washu, ameweka wazi mikakati ya kikosi hicho na kusisitiza kuwa pamoja na ushindani mkubwa uliopo katika Ligi Kuu Zanzibar, wamejipanga kupambana kufa na kupona ili kumaliza msimu wakiwa miongoni mwa timu nne bora.

Kwa sasa, Muembe Makumbi City inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 11, huku ikiwa na utofauti wa pointi nane pekee dhidi ya vinara wa ligi hiyo, Zimamoto, ambao wanakamata usukani wakiwa na pointi 19.

Akizungumza na Mwanaspoti, Jumbe amesema kuwa lengo kuu la kikosi chao ni kupata matokeo mazuri katika kila mchezo utakaofuata, hatua itakayowasaidia kujiweka katika nafasi nzuri ya kupanda juu kwenye msimamo wa ligi.

Ameongeza kuwa timu hiyo inatazamia kutumia michezo saba iliyosalia kukamilisha mzunguko wa kwanza kujikusanyia pointi za kutosha ili kufanikisha azma yao ya kuingia nne borakabla ya kusuka mikakati mipya ya duru la pili.

“Bila shaka sisi Muembe Makumbi City tunaweza kuwa mabingwa wa ligi kama tutashinda michezo yetu iliyobaki. Tusipofanya hivyo, itakuwa ngumu,” amesema Jumbe kwa kujiamini.

Sambamba na hilo, beki huyo amewaomba mashabiki na wapenzi wote wa Muembe Makumbi City kuendelea kutoa ushirikiano na kuwasapoti kwa moyo wote katika kila mchezo, akisisitiza kuwa nguvu yao ni chochezi kubwa kwa wachezaji kupambana uwanjani.

Yanga Yafunguka: Mngqithi Ataja Siri ya Kuifunga TRA United Arusha