Ligi Kuu ya Zanzibar
Michezo

Ligi Kuu Zanzibar: Kipanga FC na JKU Zaondoka na Points 6 Pemba

Vardo November 6, 2026 9:17 pm

KIPANGA FC na JKU SC zimekamilisha vyema safari yao kisiwani Pemba baada ya kuzoa alama sita muhimu katika michezo miwili ya Ligi Kuu ya Zanzibar, matokeo yaliyozifanya timu hizo kurejea nyumbani kwa kishindo.

Kipanga FC ilianza kwa kuonyesha ubora wake baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Mwenge SC, kabla ya kuendeleza moto huo kwa kuichapa Fufuni SC mabao 3-1. Matokeo hayo yameifanya Kipanga kufikisha jumla ya pointi 15 na kukaa katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi, ikilingana pointi na Muembe Makumbi inayoshika nafasi ya sita.

Kwa upande wa JKU SC, mabingwa hao watetezi wameendelea kuthibitisha ubora wao kwa kuichapa Fufuni SC mabao 2-0 na kufuatia na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mwenge SC. Alama hizo sita za Pemba zimeifanya JKU kufikisha pointi 23 na kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Zanzibar.

Makocha Wafunguka Siri ya Ushindi

Kocha Mkuu wa Kipanga FC, Khamis Hassan Makame ‘Meki’, alieleza kufurahishwa kwake na nidhamu ya wachezaji wake katika kufanikisha malengo ya safari hiyo.

“Fufuni ni timu nzuri na kuifunga kunahitaji kutumia nguvu pamoja na akili. Pamoja na kwamba walikuwa na mwenendo mbaya hivi karibuni, tukiwaambia wachezaji wetu kuwa lazima tuwaheshimu wapinzani wetu kwa sababu mpira una matokeo ya kushangaza,” alisema Kocha Meki.

Naye Kocha Mkuu wa JKU SC, Abdul-Saleh Mohamed Abdallah, alisema kuwa ingawa michezo ya Pemba haikuwa rahisi, kujituma kwa wachezaji wake kumesaidia kupata matokeo hayo mazuri.

“Tunashukuru kupata alama sita ugenini. Malengo yetu ni kupigania ubingwa msimu huu, na ushindi huu wa Pemba ni hatua muhimu kuelekea kwenye ndoto yetu,” alisema Abdul-Saleh.

Neon Heist Kukupa Ladha ya Maisha Ya Miaka ya 80 Ndani ya Meridianbet Njiku Aweka Wazi Kilichoikumba Wembe Kisiwani Unguja, Atuma Ujumbe Mzito