Siri ya Ushindi wa Simba SC Yafichuka: Clatous Chama Atoboa Siri!
KIUNGO mshambuliaji mahiri wa Simba SC, Clatous Chama, ameweka wazi siri kuu nyuma ya mafanikio ya kikosi hicho katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, akieleza kuwa mshikamano, umoja na kufanya kazi kwa pamoja ndio ngao iliyowafikisha hapo walipo.
Akizungumza hivi karibuni, staa huyo raia wa Zambia alibainisha kuwa kufikisha pointi 30 kamili baada ya kushinda michezo 10 mfululizo bila kupoteza ni ishara tosha kwamba Wekundu wa Msimbazi wako kazini kutimiza malengo yao ya kutwaa ubingwa msimu huu.
“Tumefanya vizuri kwa sababu haya ndiyo matarajio yetu kama timu na ndiyo malengo tuliyojiwekea. Katika ligi tumecheza mechi 10, hatujafungwa na zote tumeshinda. Pointi 30 ni jambo zuri sana kwetu kama wachezaji,” alisema Chama.
Licha ya rekodi hiyo ya kuvutia, fundi huyo alisisitiza kuwa kikosi hicho hakina mpango wa kubweteka. Badala yake, wameweka nguvu zote kwenye michezo mitano iliyosalia ya kumaliza mzunguko wa kwanza ili kuendelea kujitenga kileleni.
Hata hivyo, Chama alikiri kuwa mechi zijazo zitakuwa na ushindani mkubwa kutokana na kila timu pinzani kuwa na kiu ya kuwa ya kwanza kuivunja rekodi yao ya kutopoteza.
“Tumebakiwa na mechi tano sasa na kila timu inataka kuwa ya kwanza kuvunja rekodi hiyo. Simba tumejipanga kuendeleza rekodi yetu, kwa hiyo mechi hizo lazima zitakuwa ngumu,” aliongeza.
Aliitimisha kwa kuwatoa hofu mashabiki wa Simba SC na kueleza kuwa changamoto zote zinazowakabili zinawapa nguvu ya kuongeza juhudi, huku akiahidi kuwa wataendelea kupambana hadi kieleweke msimu huu.