Simba SC Ligi ya Mabingwa Afrika
Simba SC

Simba SC Kurejea Kambini: Ahmed Ally Ataja Mkakati Mzito wa Ligi ya Mabingwa Afrika

Vardo November 8, 2026 11:21 pm

Kikosi cha Simba SC kinatarajiwa kurejea kambini kesho, Jumatatu ya Novemba 9, 2026, mara baada ya kumalizika kwa mapumziko mafupi, ili kuanza rasmi maandalizi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuendeleza ushindani kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amethibitisha kuwa wachezaji wote ambao hawana majukumu katika timu zao za taifa wanatakiwa kuripoti kambini siku hiyo. Ahmed amebainisha kuwa uongozi na benchi la ufundi wamepanga maandalizi ya kina kuhakikisha kikosi kinakuwa katika kiwango cha juu kabla ya kuanza kwa mechi za kimataifa.

Kurejea huku kambini ni sehemu ya mkakati wa klabu hiyo kujiandaa na mechi ngumu za Ligi ya Mabingwa Afrika zinazotazamiwa kuanza mwezi huu, ambapo Simba inalenga kufanya vizuri zaidi.

Ahmed Ally Awatahadharisha Wachezaji Kuhusu Mapumziko

Akieleza kuhusu muda wa mapumziko waliopewa wachezaji, Ahmed alisema lengo lilikuwa ni kuwasaidia kupumzisha miili na akili zao baada ya kuwa na ratiba ya mechi mfululizo. Aliongeza kuwa baadhi ya wachezaji walitumia fursa hiyo kutembelea vivutio mbalimbali nchini ikiwemo visiwani Zanzibar na Hifadhi ya Ngorongoro.

Hata hivyo, kwa mzaha uliogubikwa na ujumbe mzito, Ahmed amewasihi wachezaji kujiepusha na shughuli zinazoweza kuwachosha miili wakati wa mapumziko, akisisitiza kuwa huu si wakati wa kwenda kijijini kutatua kero za kifamilia.

“Likizo si ya kwenda kijijini. Kijijini hawaendi kupumzika, wanaenda kusikiliza shida za wanafamilia. Sasa huo si muda wa kusikiliza shida za wanafamilia. Nenda kapumzike, nenda karelax. Ligi ya Mabingwa Afrika inakusubiri,” alisema Ahmed Ally.

Kukabili Orlando Pirates na Ligi Kuu

Mara baada ya wachezaji kukusanyika kambini, benchi la ufundi litaanza programu maalum ya mazoezi makali yanayolenga mechi yao ijayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya miamba ya Afrika Kusini, Orlando Pirates, pamoja na kuendeleza kasi yao ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Faini za Simba na Yanga Zafika Sh Milioni 10 Ali Kamwe: Yanga Ina Imani Kubwa na Fadlu, Rekodi Yake Dhidi ya Simba Inatupa Matumaini