Simba Yafunguka: Ukweli Kuhusu Deni la Kocha Davids Fadlu
SIMBA SC imeweka mambo hadharani na kufafanua kuwa sakata la kumdai aliyekuwa kocha wake, Davids Fadlu, ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha Yanga SC, si jambo jipya wala la kushangaza, bali ni suala lililoanza tangu kocha huyo alipovunja mkataba wake na klabu hiyo.
Akizungumza kuhusu suala hili, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kuwa madai hayo yanatokana na makubaliano rasmi ya kimkataba yaliyokuwepo kati ya pande hizo mbili baada ya Fadlu kuondoka klabuni hapo, akisisitiza kuwa suala hilo halihusiani kabisa na ajira yake ya sasa ndani ya Yanga SC.
Ahmed alieleza kuwa katika ulimwengu wa soka, ni jambo la kawaida kwa upande unaovunja mkataba nje ya makubaliano kulazimika kumlipa fidia upande ulioathirika. Aliongeza kuwa hata Simba imekuwa ikifuata utaratibu huo kwa kulipa wachezaji na makocha ambao mikataba yao imevunjwa na klabu.
“Baada ya Fadlu kuvunja mkataba, Simba ilifanya mazungumzo naye na kufikia makubaliano kuhusu kiasi alichotakiwa kulipa, huku kocha huyo akikubali deni hilo kabla mazungumzo hayajasimama,” alisema Ahmed.
Aliongeza kuwa mchakato huo ulipitia hatua mbalimbali, ikiwemo kipindi ambacho kocha huyo alikuwa katika klabu moja nchini Morocco na baadaye Casablanca, ambapo mazungumzo yalisimama hadi kufikia hatua ya sasa ya kutaka haki yao itendeke.
“Tunataka haki yetu na hili halihusiani na yeye kuajiriwa na timu ya hapa Tanzania. Hatujaanza kudai leo, lilikuwa deni la muda mrefu. Hatuna ugomvi na mtu yeyote, kikubwa anayevunja mkataba anatakiwa kuhakikisha kila mmoja anapata haki yake, kama sisi tunavyodai haki yetu kwa Fadlu,” alisisitiza Ahmed.