Tanzania U17 vs Costa Rica
Michezo Bongo

Maajabu Doha! Tanzania U17 yatoka nyuma 2-0 na kuilazimisha sare Costa Rica

Vardo November 21, 2026 7:19 pm

Vijana wa Tanzania U17 wameanza safari yao ya Fainali za Kombe la Dunia U17 (Qatar 2026) kwa kuandika historia ya kishujaa, baada ya kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kuilazimisha sare ya mabao 2-2 timu ya taifa ya Costa Rica katika mchezo mkali wa Kundi I uliopigwa kwenye Uwanja wa Doha Aspire Zone, Pitch 1.

Mchezo huo ulianza kwa kasi huku Costa Rica wakitumia uzoefu wao mapema na kuwashtua vijana wa Tanzania kwa mabao mawili ya haraka ndani ya robo saa ya kwanza. Jefrey Urbina ndiye aliyeanza kuandika bao la kwanza dakika ya 8, kabla ya Jorshuad Pilarte kuongeza la pili dakika ya 15, na kuifanya Tanzania kwenda mapumziko ikiwa na mlima mrefu wa kupanda.

Hata hivyo, kipindi cha pili kiligeuka kuwa cha moto kwa Costa Rica. Tanzania U17 ilirejea uwanjani ikiwa imebadilika kimbinu, ikimiliki mpira na kuishambulia ngome ya wapinzani wao bila huruma.

Juhudi hizo zilizaa matunda dakika ya 51 pale mshambuliaji hatari anayekipiga katika klabu ya Dodoma Jiji, Faraji Kayanda, alipofunga bao safi lililorejesha matumaini kwa Watanzania. Dakika nne baadaye (dakika ya 55), Tanzania ilipata nafasi ya dhahabu ya kusawazisha kwa mkwaju wa penalti, lakini Kayanda alikosa mkwaju huo.

Kukosa penalti hakukumvunja moyo nyota huyo; aliendelea kuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Costa Rica na hatimaye akasahihisha makosa yake dakika ya 73 kwa kupachika bao la kusawazisha, na kuufanya uwanja wa Aspire Zone kulipuka kwa shangwe.

Licha ya kufunga mabao mawili, Kayanda atajilaumu mwenyewe kwa kupoteza nafasi nyingine za wazi ambazo zingemfanya awe mchezaji wa pili kufunga hat-trick kwenye michuano hiyo mwaka huu, baada ya nyota wa Mali, Halidou Maïga, kufanya hivyo katika ushindi wa 3-0 dhidi ya New Zealand mnamo Novemba 20.

Takwimu za Mchezo: Tanzania Ilitawala Kila Idara

Licha ya kuambulia pointi moja, takwimu za mchezo zinaonyesha kuwa vijana wa Tanzania walikuwa bora zaidi uwanjani kuliko wapinzani wao:

  • Umiliki wa Mpira (Possession): Tanzania 59.8% – 40.2% Costa Rica

  • Mashuti Yaliyopigwa (Total Shots): Tanzania 22 – 9 Costa Rica

Nini Kinafuata?

Baada ya kuvuna alama moja muhimu katika mechi ya ufunguzi, mtihani mwingine mzito unaisubiri Tanzania U17 mnamo Novemba 24, ambapo itashuka dimbani kuwakabili mabingwa wa kihistoria, Brazil, kabla ya kuhitimisha hatua ya makundi dhidi ya Jamhuri ya Ireland mnamo Novemba 27.

Pesa za Chapchap Zipo Huku Jolly Jolly Bonanza, Zoa Maokoto Etihad Kimewaka! Fulham Yaiweka Mtegoni Man City, Mbio za Ubingwa EPL Zazidi Kuwa Ngumu