Linex Sunday Mjeda Afunguka Siri ya Kudumu Kimuziki na Sapraizi ya Feb 14
Msanii nguli wa muziki wa Bongo Fleva, Sunday Mangu maarufu kama Linex Sunday Mjeda, ni miongoni mwa wanamuziki wanaoendelea kufanya kazi kwa ustadi mkubwa bila kelele nyingi mitandaoni. Akiwa na bendi yake au wakati mwingine akipiga shoo za “chaka tu chaka,” mkali huyo bado anaendelea kukonga nyoyo za mashabiki wake ndani na nje ya Tanzania.
Katika mahojiano maalum, Linex Sunday Mjeda amefunguka mambo mengi kuhusu safari yake ya muziki, mwaliko wa tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva, pamoja na mtazamo wake kuhusu wasanii wa sasa.
Shoo Anazopiga na Uhusiano na Banana Zorro
Linex anaeleza kuwa bado anaendelea kupiga kazi kimyakimya na bendi yake, ambapo aina ya shoo hutegemea makubaliano na waandaaji—iwe ni kuimba laivu (live band) au kutumia playback.
“Ninapoletewa kazi, huwa nawauliza wanataka niende mwenyewe au nibebe vijana, na kama wanataka niimbe laivu au playback. Hata kwenye shoo za baa ambazo wengine wanakataa pesa zake, mimi naenda kutokana na namna nilivyoishi na watu, na bado napata pesa nzuri,” anasema Linex.
Aidha, amemtaja msanii mwenzake, Banana Zorro, kama mtu ambaye amekuwa akimpa shavu la kazi mara kwa mara kutokana na heshima na nidhamu aliyoijenga: “Kuna wakati kaka yangu Banana Zorro ananipa shoo za kuimba laivu, kwa wiki anaweza akaniachia hadi siku tatu. Ningekuwa sijaishi nao kwa heshima sidhani kama angefanya hivyo.”
Siri ya Nyimbo Zinazoishi
Akizungumzia kinachombeba kwenye tasnia ya muziki hadi leo, Linex Sunday Mjeda anaamini kuwa ana nyimbo zaidi ya tano ambazo hazichuji, na zinapopigwa jukwaani huamsha shangwe kama zimetoka jana.
“Nyimbo zangu zikipigwa zinakuwa na vibe kubwa na mashabiki wanaitikia. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu. Mfano nyimbo kama Mama Halima, Moyo wa Subira, Wema kwa Ubaya, na Salima bado zinaishi,” anaeleza staa huyo, huku akitolea mfano wimbo wa Kitambaa Cheupe wa marehemu King Kiki kama mfano wa nyimbo zenye ujumbe usiochuja.
Kurejea Kahama Kwenye Miaka 30 ya Bongo Fleva
Hivi karibuni, kipande cha video kikimuonyesha Linex akifanya shoo iliyojaza umati mkubwa wa watu kilisambaa mitandaoni. Linex amefafanua kuwa video hiyo ilirekodiwa mkoani Kahama miaka 13 iliyopita, na imefufuliwa sasa kuelekea tamasha kubwa la Miaka 30 ya Bongo Fleva linalotarajiwa kufanyika Kahama, Novemba 27, 2026.
“Narudi tena Kahama kwa mara nyingine kupitia Miaka 30 ya Bongo Fleva. Nawashukuru waandaji kwa kunipa heshima hii kubwa. Ingawa kwa umri wangu wengine wangeona sikustahili kuwepo, kitendo cha kaka zangu kunipa nafasi hii nakichukulia kama upendo na heshima kubwa,” alisema.
Haendeshwi na Kiki Wala Trendi za Mitandaoni
Tofauti na wasanii wengi wa kizazi kipya, Linex anasisitiza kuwa hafanyi muziki kwa kufuata upepo au trendi za mitandao ya kijamii, bali anawekeza nguvu kwenye ubora wa kazi.
-
Msimamo wake: “Ukiendekeza muziki na kutaka kuzungumziwa kila kona unaweza ukachanganyikiwa. Mimi sifuati hayo, ninachozingatia ni kufanya kazi kwa ustadi.”
-
Kuhusu video yake kutrendi: “Hata hii video ya miaka 13 iliyopita kutrendi hainipi presha. Naamini katika muziki mzuri, lakini sitaki uniendeshe akili zangu; mimi ndiye natakiwa kuuendesha muziki.”
Nidhamu, Wema na Ushauri kwa Wasanii Chipukizi
Linex anaamini kuwa ustaa unaweza kumpoteza msanii asipokuwa na hekima, lakini nidhamu na kuheshimu watu ndivyo vinavyomfanya aendelee kupata sapoti sehemu mbalimbali.
Kwa wasanii chipukizi, Linex Sunday Mjeda ametoa angalizo kali kuwa pesa na uwekezaji pekee havitoshi bila kipaji na nidhamu:
“Kuna wasanii wamekuwa wakubwa mitandaoni lakini hawana kitu, na wengine wamewekeza mamilioni ya pesa ila hawajui kuimba. Muziki ni ajira pana inayolisha familia za mameneja, wapiga picha, watayarishaji (producers), waongozaji (directors), video queens/kings na wanenguaji, hivyo lazima uheshimike kama kazi.”
Pia amegusia kuwa anapenda kusikiliza wasanii wenye uandishi wenye tija, na kufichua kuwa studio kuna wasanii wengi wa kike wenye vipaji vikubwa ambao sauti zao za vibwagizo zinasikika kwenye nyimbo za mastaa wakubwa, ingawa jamii bado haijawajua.
Sapraizi ya Februari 14 na Familia ya Waimbaji
Akihitimisha, Linex ameahidi kuwa katika kumbukumbu yake ya kuzaliwa inayofanyika Februari 14, anatarajia kuja na sapraizi kubwa yenye mtazamo wa kipekee kwenye kazi zake za muziki.
Aidha, amebainisha kuwa kipaji chake kimeanzia kwenye mizizi ya familia yake ambapo karibu kila mmoja ni mwimbaji—wakiwemo mama zake, watoto wake, na mdogo wake aitwaye David anayeimba nyimbo za injili. Ameutaja wimbo wake wa Kesho Yangu kuwa ni kisa cha kweli cha maisha yake alipopitia magumu na kujihisi mpweke kama yuko msituni peke yake.