Katika mechi zao nne walizokutana kuanzia msimu wa 2023-2024, KMC imeshinda mbili, TRA United ikipata ushindi mara moja, sare pia moja. Matokeo yapo hivi; TRA 0-1 KMC, KMC 0-2 TRA, KMC 4-2 TRA na TRA 0-0 KMC.
Saa 1:00 usiku, Namungo itakuwa mwenyeji wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Lindi, huku ikisubiriwa kwa hamu kuona Wagosi Wa Kaya wakipata ushindi wa kwanza nyumbani kwa Namungo tangu mara ya mwisho kufanya hivyo Juni 20, 2022 iliposhinda 1-0.
Coastal inayofundishwa na Mohamed Muya, inakwenda kucheza dhidi ya Namungo ikitoka kufungwa 3-0 na Azam.
Rekodi zinaonyesha, Coastal imekutana na Namungo mara 12, imeambulia ushindi mara mbili pekee na zote ikiwa ugenini. Ilifanya hivyo Novemba 22, 2019 iliposhinda 3-1 katika msimu wa kwanza Namungo kucheza Ligi Kuu Bara, kisha ikarudia Juni 20, 2022 katika ushindi wa 1-0.
Namungo imekuwa mbabe mara tano matokeo yakiwa Coastal 0-2 Namungo (Septemba 17, 2024), Namungo 1-0 Coastal )Aprili 17, 2024), Namungo 1-0 Coastal (Septemba 17, 2022), Coastal 1-3 Namungo (Januari 23, 2022) na Namungo 1-0 Coastal (Septemba 6, 2020). Sare baina yao ni tano ikiwamo ya mwisho zilipokutana uwanjani hapo Februari 23, 2025 matokeo yakiwa 0-0 na ndiyo sare pekee iliyopatikana dimbani hapo. Zingine zilikuwa nyumbani kwa Coastal Union.
Namungo mbali na kuwa na rekodi nzuri mbele ya Coastal Union, lakini mechi tano za mwisho imefanya vizuri ikishinda mbili mfululizo dhidi ya Mbeya City (1-0) na Dodoma Jiji (2-0). Kabla ya hapo, imetoka sare ya 1-1 dhidi ya Azam, ikitanguliwa kufungwa 1-0 na Mashujaa, pia ikatoka 1-1 na JKT Tanzania.
Coastal Union tano za mwisho imepoteza mbili mfululizo dhidi ya Azam (3-0) na Yanga (1-0). Ilitoka 0-0 na Mashujaa, iliichapa Mbeya City (2-0) na Matokeo ya 1-1 dhidi ya Fountain Gate.
Gepu la pointi linanogesha mechi hii kwani Coastal yenye alama tano ikishinda kwa tofauti ya mabao matatu, itakaa juu ya Namungo iliyokusanya alama nane.