BAADA YA MAUMIVU YA KIRUMBA, YANGA YAPANGA KULIPIZA KWA AZAM ZANZIBAR
BAADA ya kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB katika hatua ya nusu fainali, Yanga SC sasa imehamishia nguvu zake zote kwenye mbio za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mabingwa hao watashuka dimbani Juni 24, 2026 katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kuikaribisha Azam FC katika mchezo muhimu ambao unaweza kuwa na athari kubwa kwenye vita ya ubingwa.
Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto, amesema matokeo ya mchezo wa nusu fainali yamebaki kuwa historia na kwamba kikosi chao kimejipanga kuhakikisha kinarejea kwenye njia ya ushindi katika mechi za ligi zilizobaki.
Mwamnyeto amesema hawataendelea kulia na matokeo ya kuondolewa kwenye Kombe la Shirikisho, badala yake wameamua kuangalia mbele na kupambana kwa ajili ya kutimiza malengo yaliyosalia msimu huu.
“Haikuwa bahati kwetu, lakini hayo ni matokeo ya mpira wa miguu, tumeshapoteza na sasa tunaelekeza nguvu zetu zote katika mechi zilizobaki za ligi,” amesema Mwamnyeto.
Aliongeza kuwa benchi la ufundi tayari limefanya tathmini ya mchezo uliopita na kubaini maeneo yaliyohitaji maboresho, jambo ambalo linaipa timu nafasi ya kurejea ikiwa imara zaidi katika mchezo dhidi ya Azam FC.
Kwa mujibu wa nahodha huyo, Yanga inaamini bado ina nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kwamba ushindi dhidi ya Azam FC utakuwa hatua muhimu katika kufanikisha azma hiyo.