Home Habari za michezo MPANZU AFUNGUKA MAZITO, ANACHOPITIA NI…

MPANZU AFUNGUKA MAZITO, ANACHOPITIA NI…

0

KIUNGO wa Simba SC, Elie Mpanzu, amefunguka na kukata mzizi wa fitna kuhusu taarifa zinazomhusisha na kuwa na mapenzi na wapinzani wao wa jadi, Yanga SC.

Nyota huyo amesema anachokipitia kwa sasa ni kipindi kigumu cha kawaida kwa mchezaji, lakini anaamini atarejea katika ubora wake wa zamani.

Kauli ya Mpanzu inakuja kufuatia madai kwamba kushuka kwa kiwango chake kunatokana na kutokuwa na furaha ndani ya Simba pamoja na madai ya kuwa na mapenzi na Yanga.

Amesisitiza kuwa maneno hayo hayana ukweli wowote na yamekuwa yakisambazwa bila msingi.

“Nipo kama wachezaji wengine, napitia kipindi kigumu ambacho ni sehemu ya maisha ya soka. Lakini wapo watu wamegeuza hilo kuwa fursa ya kusema maneno ambayo sijawahi kuyazungumza na mtu yeyote,” amesema Mpanzu.

Ameweka wazi kuwa yeye ni mchezaji halali wa Simba na anaipenda timu hiyo kwa moyo wake wote, huku akibainisha kuwa kuna mambo binafsi yaliyomtikisa kwa muda mfupi.

“Mimi ni mchezaji wa Simba na ninaipenda sana timu yangu. Ni kweli kuna mambo binafsi yametokea na yamenitingisha kidogo, lakini naamini nitakuwa sawa na kurudi kama zamani,” ameongeza.

Katika kuonyesha kuwa hali hiyo ni ya kawaida kwa mchezaji yeyote, Mpanzu alimtolea mfano , Fiston Mayele, akisema kuwa hata yeye amewahi kupitia kipindi cha ukame wa mabao lakini baadaye akarudi kwenye kiwango chake.

“Mayele hajafunga kwa muda mrefu, lakini hilo hutokea kwa mchezaji yeyote. Baadaye unarudi kwenye ramani. Naamini hata mimi nitarudi kwenye ubora wangu. Naomba mashabiki wa Simba wasimame na mimi katika kipindi hiki kigumu na waepuke kusikiliza maneno ya watu,” amesisitiza Mpanzu.