MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameibua mjadala mkubwa mitandaoni baada ya kumpachika jina la utani mshambuliaji wa timu hiyo, Libasse Gueye, akimuita “MRI” kufuatia kiwango cha juu alichoonyesha dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Yanga SC.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Ahmed alichapisha picha ikimuonyesha Gueye akiwa na mpira huku akizungukwa na wachezaji sita wa Yanga waliokuwa wakijaribu kumkabili.
Miongoni mwao walionekana Mudathir Yahya, Prince Dube, Mohammed Damaro na Duke Abuya, lakini wote walishindwa kuuzuia mfululizo wa chenga na kasi ya mshambuliaji huyo.
Akiambatanisha picha hiyo, Ahmed aliandika kwa utani: “M.R.I kifaa cha kisasa cha kupima umri kikiendelea na majukumu yake.”
Kauli hiyo iliwachekesha mashabiki wengi na kuzua tafsiri mbalimbali, wengi wakihusisha ubunifu wa Gueye na mashine ya kitabibu ya MRI wakimaanisha kuwa aliwachambua wapinzani wake mmoja baada ya mwingine kwa ustadi wa hali ya juu.
Kitaalamu, MRI (Magnetic Resonance Imaging) ni kipimo cha kisasa cha kitabibu kinachotumia nguvu ya sumaku na mawimbi ya redio kupiga picha za ndani ya mwili kwa uwazi mkubwa bila kutumia mionzi ya X-ray.
Kwa upande wa Ahmed, tafsiri ya “MRI” ilikuwa ya kimchezo zaidi kuliko kitabibu, alimaanisha kuwa Gueye aliwasoma mabeki wa Yanga kwa umakini na akawachambua kwa ustadi kisha kupenya katikati yao bila huruma, kana kwamba alikuwa anafanya uchunguzi wa kina kabla ya kutoa majibu.
Kauli hiyo imeongeza presha ya ushindani kati ya miamba hiyo ya soka nchini, huku mashabiki wakichukua nafasi hiyo kuendeleza utani wa jadi wa Kariakoo. Bila shaka, jina la “MRI” linaweza kubaki midomoni mwa wengi iwapo Gueye ataendelea kuonyesha makali yake uwanjani.