Habari za michezo
PACOME AREJEA, PEDRO AONGEZA NGUVU YANGA
Vardo
March 11, 2026
4:31 pm
KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Pedro Goncalves ameweka wazi kuwa hana nafasi ya kufanya masihara linapokuja suala la pointi tatu katika mchezo wao wa kesho wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akisisitiza kuwa ameandaa kikosi imara kitakachopambana kuhakikisha wanapata ushindi muhimu.
Timu hiyo imeondoka leo asubuhi kuelekea jijini Dodoma kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Tanzania Prisons utakaochezwa kesho katika Uwanja wa Jamhuri Stadium.
Mchezo huo ni sehemu ya ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo Yanga inalenga kuendelea kukusanya alama muhimu katika mbio za ubingwa.
Pedro amesema licha ya kuwepo kwa sintofahamu kuhusu mahali mchezo huo ungechezwa hadi jana usiku ratiba ilipothibitishwa, hilo halijapunguza maandalizi ya kikosi chake.
Ameeleza kuwa wachezaji wako tayari kupambana ili kuhakikisha wanarejea na alama zote tatu.
Kocha huyo amefafanua kuwa kikosi kitakachoanza mchezo huo huenda kikawa na mabadiliko kadhaa kutokana na hali ya baadhi ya wachezaji, huku akibainisha kuwa wapo waliokuwa majeruhi ambao tayari wameanza kurejea kikosini.
“Akili na nguvu zetu zote zimeelekezwa kwenye kupata alama tatu dhidi ya Tanzania Prisons. Tupo tayari kwa mchezo huo na kikosi kitakuwa na mabadiliko kadhaa, kuna baadhi ya wachezaji majeruhi lakini pia wapo waliopona, akiwemo Pacome Zouzoua ambaye anaweza kucheza kesho,” amesema kocha huyo.
Ameongeza kuwa anatarajia mchezo huo kuwa mgumu kwa sababu wapinzani wao pia wanahitaji alama muhimu, Yanga italazimika kupambana kwa nguvu ili kupata matokeo chanya kabla ya kuelekeza nguvu zao katika mchezo mwingine dhidi ya Azam FC.