Yanga SC

YANGA YAZAMA KWENYE MAZUNGUMZO MAZITO YA KUWABAKISHA MASTAA WAKE

Vardo June 23, 2026 4:46 pm

UONGOZI wa Young Africans SC umesema umeweka mikakati kabambe ya usajili kuelekea msimu ujao wa 2026/27, ambapo kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha wachezaji waliopo kwenye kikosi wanaongezewa mikataba kabla ya kuanza kusajili nyota wapya.

Mssemaji wa klabu hiyo, Ali Kamwe amesema kwa sasa uongozi uko kwenye mazungumzo na wachezaji ambao mikataba yao inafikia ukomo ili kuhakikisha wanaendelea kubaki ndani ya kikosi hicho.

Kamwe amesema mazungumzo hayo yanalenga kuimarisha msingi wa timu kabla ya kufanya maboresho mengine yatakayofuata katika dirisha la usajili la msimu ujao.

Amefafanua kuwa baada ya kukamilisha zoezi la kuongeza mikataba kwa wachezaji wanaohitajika kubaki, ndipo uongozi utahamia katika hatua ya kusajili wachezaji wapya watakaosaidia kuimarisha kikosi kwa ajili ya changamoto za msimu ujao.

Katika hatua nyingine, Kamwe amekanusha kuwepo kwa mazungumzo yoyote kati ya Yanga na makocha wapya kwa ajili ya kujiunga na klabu hiyo, akisisitiza kuwa uongozi una imani kubwa na benchi la ufundi lililopo kwa sasa.

Ameongeza kuwa kwa sasa nguvu kubwa ya uongozi imeelekezwa kwenye maandalizi ya mechi tano zilizobaki za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Amewataka mashabiki na wanachama wa Yanga kuendelea kuiunga mkono timu kwa kujitokeza kwa wingi viwanjani na kuwaombea wachezaji ili wafanikishe malengo ya kubakisha heshima ya klabu na kutwaa mataji yaliyosalia msimu huu.

MUDA WA MABINGWA WA DUNIA UMEFIKA MKENYA KULAMBA DILI PAMBA JIJI