SIMBA YATAMKA WAZI KIKWAZO KIKUBWA NI AZAM FC
MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kuwa kwa mtazamo wake ilikuwa rahisi zaidi kwa Simba kucheza dhidi ya Yanga kuliko Azam FC katika fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.
Simba SC imekuwa timu ya kwanza kutinga hatua ya fainali baada ya kuiondoa Coastal Union, huku Azam FC ikifuzu kufuatia ushindi wake dhidi ya Yanga katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa mwishoni mwa wiki.
Fainali ya michuano hiyo inatarajiwa kuchezwa Julai 4, 2026, ingawa hadi sasa mamlaka husika bado hazijatangaza rasmi uwanja utakaotumika kwa ajili ya mchezo huo mkubwa.
Akizungumza kuhusu wapinzani wao wa fainali, Ahmed amesema wamepokea kwa tahadhari kubwa kufuzu kwa Azam FC, akieleza kuwa timu hiyo imeonyesha kuwa mpinzani mgumu kwa Simba msimu huu tofauti na timu nyingine ambazo wangekuwa na matumaini makubwa ya kuzifunga.
“Kwa mtazamo wangu, nafasi yetu ya kuifunga Azam FC ni takribani asilimia 60, lakini dhidi ya timu nyingine yoyote tungekuwa na nafasi kubwa zaidi ya kupata ushindi.
Ndiyo maana baada ya Azam kutinga fainali tumeona tumekosa fainali nyepesi na sasa tunakutana na mpinzani mgumu zaidi,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa takwimu zinaonyesha Simba imekuwa na matokeo mazuri zaidi dhidi ya Yanga kuliko Azam FC msimu huu. Ahmed alisema Simba iliifunga Yanga katika Kombe la Muungano, kisha ikapata sare katika michezo mingine iliyofuata.
Kwa upande wa Azam FC, Ahmed amesema timu hiyo imekuwa na rekodi bora dhidi ya Simba msimu huu baada ya kushinda mchezo mmoja na kutoka sare katika mwingine, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa Azam ni miongoni mwa timu ngumu kwa Simba kwa sasa.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa Simba itaingia fainali ikiwa na lengo la kupambana na kuhakikisha inatwaa taji hilo.